Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wizara ya Viwanda na Biashara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuendelea kuimarisha sekta za viwanda na biashara nchini pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 22, 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 104.1 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida.
Amesema fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha Shilingi bilioni 78.0 kwa ajili ya mishahara ya watumishi huku Shilingi bilioni 26.0 zikitengwa kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji wa wizara na taasisi zake.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri Kapinga amesema jumla ya Shilingi bilioni 33.6 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya viwanda na biashara.
Amesema fedha zote za maendeleo zinazotarajiwa kutumika katika mwaka huo wa fedha zinatokana na vyanzo vya ndani vya Serikali, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya viwanda na biashara nchini.
Waziri huyo amesema bajeti hiyo inalenga kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani na kuimarisha uwezo wa ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha, amesema serikali itaendelea kuchochea ukuaji wa biashara kwa kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi pamoja na kupanua fursa za masoko ya bidhaa za Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.
Waziri Kapinga amesema kupitia bajeti hiyo, wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na mipango mbalimbali inayolenga kuongeza ajira, mapato ya serikali na mchango wa sekta ya viwanda na biashara katika ukuaji wa uchumi wa taifa.


No comments:
Post a Comment