Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza uwezo wa utoaji huduma kwa kununua vifaa vya kisasa vya uhakiki wa vipimo pamoja na kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi mpya katika mikoa ya Lindi na Songwe.
Hayo yameelezwa bungeni na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Kapinga amesema hadi Aprili 2026, usanifu na michoro ya majengo ya ofisi hizo imekamilika na hatua inayofuata ni kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi.
Aidha, amesema WMA imenunua vifaa mbalimbali vya kisasa vya TEHAMA ikiwemo laptop 35, desktop 28, scanner mbili, multifunction printer 20, photocopier mbili pamoja na colour printer moja kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na huduma kwa wananchi.
Katika kuongeza uwezo wa kitaalam wa uhakiki wa vipimo, Wakala pia umekamilisha ununuzi wa vifaa 72 vya kitaalam vinavyotumika katika ukaguzi na uhakiki wa vipimo mbalimbali.
Vifaa hivyo ni pamoja na digital thermometer, CNG dispensing pump verifier, electronic balances 31, mass comparator mbili, flow meters nne, proving tanks 11, pressure gauges tisa, portable legal metrology test kit for field inspectors 40 pamoja na legal metrology test kits for verifying high precision balances 20.
Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, upatikanaji wa vifaa hivyo utaongeza wigo wa huduma za uhakiki wa vipimo katika maeneo mapya na kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu zaidi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali kupitia WMA inaendelea kukabiliana na changamoto ya matumizi ya “Lumbesa” katika biashara ya mazao ya kilimo nchini.
Amesema Sheria ya Vipimo Sura ya 340 inaelekeza kuwa mazao yaliyofungashwa kwa uzito hayapaswi kuzidi kilogramu 100 pamoja na kiwango himilivu cha asilimia tano, huku ikisisitiza matumizi ya mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo angalau mara moja kwa mwaka.
Kapinga amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imeendesha operesheni tisa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa na Njombe.
Kupitia operesheni hizo, magari 2,500 yaliyokuwa yakisafirisha mazao yalikaguliwa ambapo magari 2,419 yalibainika kufuata taratibu za sheria kwa kubeba mazao yaliyofungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu 100.
Hata hivyo, magari 81 yalikutwa na makosa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340 na hatua mbalimbali zilichukuliwa dhidi ya wahusika ikiwemo kutozwa faini ya papo kwa papo pamoja na kuamriwa kufungasha upya mazao hayo.
Waziri Kapinga amesema operesheni hizo zinaendelea kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia ofisi za Wakala wa Vipimo zilizopo nchi nzima kwa lengo la kutokomeza kabisa changamoto ya “Lumbesa”.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha vituo vya muda 5,050 katika maeneo ya kata, mitaa na vijiji kwa ajili ya huduma za uhakiki wa vipimo.
Pia amesema baadhi ya halmashauri za miji na wilaya zikiwemo Mpanda, Kasulu na Kibondo zimetunga sheria ndogo za ushuru wa mazao zinazosisitiza matumizi ya mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo katika biashara ya mazao.


No comments:
Post a Comment