TANZANIA YAIMARISHA BIASHARA YA KIMATAIFA, MAUZO NJE YA NCHI YAFIKIA DOLA BILIONI 10 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 22, 2026

TANZANIA YAIMARISHA BIASHARA YA KIMATAIFA, MAUZO NJE YA NCHI YAFIKIA DOLA BILIONI 10


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Biashara ya Tanzania katika soko la kimataifa imeendelea kuimarika ambapo thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi imeongezeka kwa asilimia 16 na kufikia dola za Marekani milioni 10,080.9 mwaka 2025 kutoka dola milioni 8,702 mwaka 2024, hatua inayotajwa kuchochewa na kuimarika kwa mazingira ya biashara, upatikanaji wa masoko na ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kapinga amesema bidhaa zilizouzwa kwa wingi katika masoko ya nje ni pamoja na ufuta, tumbaku, mbaazi, kahawa, pamba, parachichi, samaki, dhahabu, makaa ya mawe pamoja na bidhaa za viwandani kama mabati na vigae.

Amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na kupunguza vikwazo vya usafirishaji wa bidhaa ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.

Kwa upande wa bidhaa zinazoingizwa nchini, Waziri huyo amesema thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje iliongezeka hadi dola za Marekani milioni 16,031.3 mwaka 2025 kutoka dola milioni 15,684.5 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 2.2.

Katika soko la Umoja wa Ulaya (EU), Waziri Kapinga amesema mauzo ya Tanzania yaliongezeka kwa asilimia 37.5 kutoka dola milioni 686.3 mwaka 2024 hadi dola milioni 943.8 mwaka 2025 kutokana na kuongezeka kwa ubora wa bidhaa na mahitaji ya bidhaa za kikaboni.

Aidha, amesema Tanzania iliendelea kufanya vizuri katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo mauzo ya bidhaa yaliongezeka kwa asilimia 8.7 na kufikia dola milioni 1,264.6 mwaka 2025 kutoka dola milioni 1,163.8 mwaka 2024.

Kwa upande wa SADC, Waziri Kapinga amesema mauzo ya bidhaa yaliongezeka kwa asilimia 19.4 na kufikia dola milioni 3,545 mwaka 2025, huku bidhaa za kilimo na viwandani zikiendelea kuongoza katika soko hilo.

Amesema biashara na Bara la Asia pia imeendelea kukua ambapo mauzo ya Tanzania kwenda China, India na Japan yalifikia dola milioni 3,213.2 mwaka 2025 kutoka dola milioni 2,840.3 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 13.1.

Waziri Kapinga amesema serikali itaendelea kuimarisha diplomasia ya biashara, kutafuta masoko mapya na kuboresha ubora wa bidhaa za Tanzania ili kuongeza mapato ya taifa, ajira na ushindani wa bidhaa za ndani katika masoko ya kikanda na kimataifa.

No comments:

Post a Comment