Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wizara ya Viwanda na Biashara imesema itaelekeza nguvu katika utekelezaji wa vipaumbele vinane vya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga amesema serikali itaendelea kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda nchini ili kuongeza thamani ya mazao na malighafi zinazozalishwa hapa nchini.
Waziri Kapinga amesema moja ya vipaumbele vikuu vya wizara hiyo ni kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kielelezo ikiwemo mradi wa Liganga na Mchuchuma, Magadi Soda Engaruka pamoja na mradi wa Maganga Matitu ambayo inalenga kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwandani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amesema wizara pia itaendelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani kwa kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji pamoja na kuendeleza miundombinu ya maeneo ya viwanda na kongani za viwanda kwa ajili ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Katika upande wa biashara, Waziri Kapinga amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi, kurahisisha taratibu za biashara na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi ili kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania.
Aidha, amesema wizara itaendelea kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini kupitia diplomasia ya biashara, ushiriki katika maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbalimbali duniani.
Waziri huyo amesema serikali pia itaendelea kuimarisha usimamizi wa ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa nchini zikiwemo bidhaa za chakula, vipodozi, dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakidhi viwango vya ushindani katika soko la kimataifa.
Vilevile, amesema wizara itaendelea kuratibu majadiliano ya biashara baina ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa sambamba na kusimamia utekelezaji wa sera mpya za maendeleo ya viwanda na ujasiriamali zilizofanyiwa mapitio mwaka 2025.
Waziri Kapinga amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo unalenga kuongeza ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya serikali, kukuza uchumi wa taifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa viwandani na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.


No comments:
Post a Comment