
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha mifumo ya vipimo kama sehemu ya kuendeleza uchumi wa viwanda na biashara ili kuifanya nchi iweze kushindana kikamilifu kimataifa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo ameyasema hayo Mei 20, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Safina House uliopo jijini Dodoma.
Mhe. Londo amesema kuwa vipimo ndivyo vinavyowezesha kutambua kwa usahihi ukubwa na asili ya changamoto zinazokusudiwa kutatuliwa ambapo bila taarifa zinazopimika na kuthibitishwa, kuna hatari ya kutunga sera zisizolenga tatizo halisi hali ambayo inaweza kusababisha upotevu wa muda na rasilimali za Taifa.
“Katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia, sekta ya vipimo ina mchango mkubwa katika kuchochea ubunifu, kuongeza tija viwandani na kulinda afya na usalama wa wananchi. Hivyo, ni wajibu wetu kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya vipimo, maabara na wataalamu wenye ujuzi ili Tanzania iweze kushindana kikamilifu kimataifa”, amesema Mhe. Londo.
Ameongeza kuwa, mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea usahihi wa vipimo vinavyotumika na hakuna viwanda vinavyoweza kushindana kimataifa bila vipimo sahihi; hakuna biashara ya kimataifa bila uhakiki wa vipimo na hakuna huduma bora za afya bila vipimo vinavyoaminika.
Vile vile, amefafanua kuwa maadhimisho hayo si tu ya kitaaluma, bali ni sehemu ya msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hivyo, ili kufikia malengo hayo, nchi inahitaji sera imara, zinazotekelezeka, zinazopimika na zinazoakisi uhalisia wa kiuchumi, kiteknolojia na kijamii.
Aidha, ametoa wito kwa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuendelea kusimamia haki katika matumizi ya vipimo, kuhakikisha uadilifu katika biashara pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kuimarisha mifumo ya vipimo vya kisayansi, maabara za kitaifa, ithibati na ulinganifu wa vipimo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Pia, ametoa rai kwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuendeleza na kuboresha programu za mafunzo zinazohusiana na vipimo, tathmini ya ubora na sera ili kuandaa wataalamu wanaoweza kuunganisha sayansi, sera na utekelezaji.
Siku ya Vipimo Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Mei, ikiwa ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Kimataifa wa Mita mwaka 1875. Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu ya “Sayansi ya vipimo isaidie kuleta imani katika uandaaji wa sera”.





No comments:
Post a Comment