SERIKALI YASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUIMARISHA USALAMA MIPAKANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 19, 2026

SERIKALI YASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUIMARISHA USALAMA MIPAKANI



Serikali imesema hali ya ulinzi na usalama katika mipaka yote ya Tanzania yenye urefu wa kilomita 5,923.41 inayohusisha nchi kavu, anga na maji inaendelea kuwa shwari, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mipaka hiyo inalindwa ipasavyo.

Hayo yameelezwa leo Mei 19, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Dkt. Rhimo Nyansaho, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Dkt. Nyansaho amesema licha ya kutokuwepo matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani kati ya Tanzania na nchi jirani, bado kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji kuendelea kushughulikiwa ikiwemo uharibifu wa alama za mipaka, ubovu wa barabara za ulinzi na migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi jirani.

Amesema mpaka wa Tanzania na Burundi wenye urefu wa kilomita 468.85 unaendelea kuwa salama licha ya changamoto za uharibifu wa alama za mpaka na barabara za ulinzi, huku Wizara kupitia JWTZ ikiendelea kuimarisha doria na shughuli za ulinzi.

Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Dkt. Nyansaho amesema hali ya usalama ni shwari lakini mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC kati ya Jeshi la nchi hiyo na kundi la M23 yanaendelea kuleta changamoto za kiusalama katika eneo hilo.

Amesema kundi la M23 limeendelea kushikilia maeneo ya kimkakati katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini ikiwemo miji ya Goma, Bukavu na Uvira, hali inayoongeza tahadhari za kiusalama katika mpaka huo.

Kuhusu mpaka wa Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilomita 1,187, Waziri huyo amesema hali ni tulivu na kazi ya kuimarisha alama za mpaka inaendelea kufanywa kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Tanzania na Kenya.

Aidha, amesema mpaka wa Tanzania na Malawi unaendelea kuwa salama licha ya kuwepo mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa, huku Serikali ikiendelea kutumia njia za kidiplomasia kupitia Tume Maalum ya Usuluhishi inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano.

Katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, Waziri Nyansaho amesema changamoto kubwa ni uwepo wa kikundi cha kigaidi cha Ansar Al-Sunna Wal Jamaah (ASWJ) katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji kinachopakana na Mkoa wa Mtwara. Amesema JWTZ imeendelea kuimarisha ulinzi na uwezo wa vikosi vinavyolinda mpaka huo.

Pia amesema mipaka ya Tanzania na Rwanda, Uganda pamoja na Zambia inaendelea kuwa salama licha ya changamoto za uchakavu wa alama za mipaka na uingizaji haramu wa mifugo katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali itaendelea kushirikiana na nchi jirani pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha mipaka ya Tanzania inaendelea kuwa salama na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.



No comments:

Post a Comment