SERIKALI YAIMARISHA ULINZI WA ANGA NA BAHARI DHIDI YA MATISHIO YA KIUSALAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 19, 2026

SERIKALI YAIMARISHA ULINZI WA ANGA NA BAHARI DHIDI YA MATISHIO YA KIUSALAMA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 


Serikali imesema hali ya ulinzi na usalama wa anga la juu pamoja na mpaka wa Bahari ya Hindi inaendelea kuwa shwari, huku hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa kukabiliana na matishio yanayotokana na mabadiliko ya teknolojia na uhalifu wa kimataifa.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, amesema Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa vyombo vya ulinzi katika kulinda anga la juu la Tanzania.

Dkt. Nyansaho amesema pamoja na hali ya usalama kuwa tulivu, anga la juu limeendelea kuwa na changamoto kutokana na ongezeko la matumizi ya teknolojia za kisasa ambazo zimeifanya hali ya kiusalama kuwa ya kutabirika kwa kiwango kidogo.

Amesema Wizara ya Ulinzi na JKT kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine imeendelea kujiimarisha kwa kuongeza vifaa, zana, wataalam pamoja na kutoa mafunzo na semina mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa salama dhidi ya matishio ya anga la juu.

Kuhusu usalama wa mpaka wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa Nautical Miles 864.376 unaohusisha mipaka ya Tanzania na nchi za Comoros pamoja na Shelisheli, Waziri huyo amesema hali ya usalama imeendelea kuwa shwari bila kuwepo matukio yoyote yaliyohatarisha usalama wa taifa katika kipindi husika.

Amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kufanya doria za mara kwa mara katika eneo la Bahari ya Hindi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kukabiliana na vitendo vya uharamia, wahamiaji haramu, uvuvi haramu, biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na matishio ya ugaidi.

Kwa mujibu wa Dkt. Nyansaho, Serikali itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha mipaka ya anga na bahari inalindwa ipasavyo sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kuvuka mipaka.

No comments:

Post a Comment