Na Mwandishi Wetu, Masvingo - Zimbabwe
TANZANIA imesema itaendelea kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI) katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa tahadhari za mapema na kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, wakati wa mkutano wa maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Mei 11, 2026 mjini Masvingo, Zimbabwe.
Alisema matumizi ya AI yatasaidia uchakataji na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali zinazoripotiwa kuhusu masuala ya maafa nchini, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa Serikali katika kufanya maamuzi ya haraka wakati wa majanga.
“Matumizi ya teknolojia ya Akili Unde yatawezesha uchambuzi wa taarifa kwa haraka, kutabiri hatari zinazoweza kujitokeza na kusaidia hatua za mapema za kukabiliana na maafa,” alisema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi alisema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika maeneo muhimu yatakayosaidia kuwa na usimamizi wenye tija wa maafa ikiwemo utafiti wa kisayansi, matumizi sahihi ya Akili Unde, ushirikiano katika uhifadhi wa taarifa za matukio pamoja na matumizi ya menejimenti ya maarifa.
Aidha alisema Tanzania imeendelea kuwa mfano katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kutokana na uwezo wake wa kuratibu na kusimamia maafa kwa mafanikio huku ikiendelea kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa na kurejesha hali pindi majanga yanapotokea.
Alifafanua kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na uwepo wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema ambacho hufanya kazi saa 24 kupokea, kufuatilia na kuchambua taarifa za majanga kwa wakati halisi.
“Kituo cha Operesheni ya Maafa kimekuwa msaada mkubwa kwani kimerahisisha upatikanaji wa taarifa za mapema, uchambuzi wa takwimu za wakati halisi na upangaji wa mikakati ya kurejesha hali pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujiandaa na kukabiliana na maafa,” alisisitiza.





No comments:
Post a Comment