
Benki ya Dunia (WB) imeipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, ikieleza kuwa nchi imekuwa kinara wa kuigwa barani Afrika katika matumizi ya mfumo wa malipo kwa matokeo (P4R).
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma katika kikao kilichowakutanisha Menejimenti ya Wizara ya Maji na ujumbe kutoka Benki ya Dunia kilicholenga kujadili maendeleo ya sekta ya maji nchini pamoja na hatua za kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Kanda wa Benki ya Dunia kwa Mashariki na Kusini mwa Afrika, Anna Wellenstein, amesema Tanzania imefanikiwa kutekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali ya maji vijijini inayofadhiliwa na WB kupitia mfumo wa P4R.
Amesema mafanikio hayo yameonesha utekelezaji mzuri wa Mpango Mkakati wa Mtandao wa Taifa wa Usambazaji Maji, huku yakichochea upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa vijijini.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hali inayowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini.
Aweso ameielekeza Menejimenti ya Wizara ya Maji kuendelea kuimarisha ushirikiano na Benki ya Dunia ili kuhakikisha miradi yote ya maji inakamilika kwa wakati na kuendelea kusogeza mbele azma ya Serikali ya kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030.
Aidha, kikao hicho kilijadili mafanikio ya ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Benki ya Dunia pamoja na vipaumbele vya hatua inayofuata katika maendeleo ya sekta ya maji kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ujumbe wa Benki ya Dunia ulioshiriki kikao hicho ulihusisha wataalamu mbalimbali akiwemo Soma Ghosh Moulik, Zhimin Mao, Ernest Ruzindaza pamoja na Luth Kennedy-Walker.



No comments:
Post a Comment