Na Neema Mbuja na Kassim Nyaki, Dodoma
Imeelezwa kuwa Tanzania ni miongoni kwa nchi za awali katika bara la Afrika zilizopewa hadhi ya kimataifa ya Kijiopaki na UNESCO kutokana na mchango mkubwa kupitia Jiopaki ya Ngorongoro Lengai iliyopelekea Serikali kujenga makumbusho ya kisasa ya jiopaki (Urithi Geopark Museum) iliyojengwa na serikali wilaya ya Karatu Mkoani Arusha na kuzinduliwa mwaka 2025.
Akiwaslisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema makumbusho hayo ni sehemu ya Jiopaki ya Ngorongoro Lengai ambayo imejengwa kwa lengo la kutoa elimu kuhusu sayansi ya miamba, volkano, na historia ya mazingira, na ni ya pekee katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara
Amesema kupitia makumbusho hayo Watalii na wadau wanaotembelea jengo hilo wanapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo muonekano wa dunia miaka mingi iliyopita na ilivyo sasa, maumbile asilia yanayopatikana katika ukanda wa bonde la ufa, kujionea mwamba wenye umri wa miaka milioni tatu iliyopita unaopatikana hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai, sambamba kujifunza tamaduni za makabila ya Wahadzabe, Wairaq, Wadatoga na Wamasai pamoja, kupima uwezo wa kutambua sauti za wanyamapori, kushindana mbio kwa kutumia baiskeli na wanyamapori ndani ya makumbusho na mengine mengi.
Makumbusho hii inayosimamia na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa sehemu ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) lenye hadhi tatu zinazotambulika na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo hadhi hizo ni Eneo la Hifadhi ya Mazingira na Binadamu (Man and Biosphere Reserve 1981), Eneo la Urithi Mchanganyiko wa Asili na Kitamaduni (Mixed World Heritage 2010) na hadhi ya tatu Eneo la Hifadhi ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark 2018) ambazo Tanzania ni nchi ya pili kupata hadhi hiyo ikitanguliwa na nchi ya Morocco
Tanzania Ina Jumla ya maeneo ya malikale 158 na maeneo 7 yametambuliwa kama urithi wa dunia






No comments:
Post a Comment