TANZANIA YAJIPANGA KUWA MZALISHAJI MKUBWA WA MADINI KINYWE (GRAPHITE) DUNIANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 28, 2026

TANZANIA YAJIPANGA KUWA MZALISHAJI MKUBWA WA MADINI KINYWE (GRAPHITE) DUNIANI



Na Mwandishi Wetu Ruangwa, Lindi


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kwamba Tanzania inajipanga kuwa mmoja ya wazalishaji wakubwa Duniani wa madini kinywe(𝙂𝙧𝙖𝙥𝙝𝙞𝙩𝙚) kupitia Kampuni 30 zinazomiliki Leseni za kati na kubwa za uchimbaji wa madini hayo na hivyo kutoa ushindani wa kiuzalishaji kwa nchi ya China ambayo ndio inaongoza kwa uzalishaji wa madini hayo duniani kwa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka.

Mhe Mavunde ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 Wilayani Ruangwa, Lindi aliposhiriki katika hafla ya utiaji saini wa mikataba wa ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kwa ajili ya mradi mkubwa wa uchimbaji madini kinywe na kubainisha kuwa kuanza kwa uchimbaji mkubwa wa madini mkakati ya kinywe (graphite) kunaiweka Tanzania kwenye dira ya duniani kama Nchi ya kimkakati katika uzalishaji wa madini hayo muhimu kwenye utengenezaji wa betri za magari ya umeme.

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuijenga na kuifanya nchi yetu ya Tanzania kama Taifa lenye dira wazi ya kiuchumi, mazingira rafiki ya uwekezaji na usimamizi imara wa rasilimali zake," amesema Waziri Mavunde

Amesema tukio la leo ni matokeo ya dira na maono hayo thabiti ya Mhe Rais ambayo yameendelea kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya wawekezaji ambayo ina sera na Sheria zinazoeleweka na kutabirika.

Pia, Mhe.Mavunde amefafanua kwamba kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya sita Duniani kwa uzalishaji wa madini kinywe ambapo kwa mwaka uzalishaji wa Tanzania ni tani 25,000 kwa kampuni mbili tu zilizoanza uzalishaji mkubwa za Lindi Jumbo na God Mwanga-Tanga huku zingine 28 zikiwa katika hatua mbalimbali za kuanza uzalishaji.

Mhe Mavunde amewataka wamiliki wa Leseni 28 za uchimbaji madini kinywe kuhakikisha wanaanza uzalishaji mapema kama sheria inavyoelekeza ili kuepuka kufutuwa leseni hizo.

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa dunia kwa sasa inapita kwenye mageuzi makubwa ambapo madini kinywe ni msingi wa kesho kwani upatikanaji wake ni kichocheo kikubwa katika uzalishaji wa nishati safi kwa kusaidia utengenezaji betri za magari ya umeme.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 82 unataraji kuzalisha madini kinywe tani 40,000 kwa mwaka katika kipindi cha uhai miaka 24 ya mgodi ambapo zaidi ya ajira 300 zimezalishwa hadi sasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye sekta ya madini, Prof. Sifuni Mchome ameeleza kuwa miongoni mwa faida ambazo Serikali itapata kupitia kusaini mikataba hiyo ya ubia ni pamoja na udhibiti wa fedha na uhakika wa mapato kutokana na uwekezaji huo na fursa za ajira kwa watanzania.

Prof. Mchome amebainisha kuwa kupitia
makubaliano hayo yaliyotiwa saini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itamiliki asilimia 16 ya hisa huru zisizohafifishwa thamani (non-dilutable free carried interest shares), huku Kampuni ya Lindi Jumbo Limited ikimiliki asilimia 84 ya hisa katika kampuni ya ubia.

Awali, akieleza maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Lindi Jumbo Limited, Bw. Andrew Cunningham amebainisha kuwa pamoja na upanuzi wa uzalishaji wa mgodi huo, wataendelea kufanya utafiti ili kubaini mashapo zaidi ambayo yatarefusha maisha ya mgodi na kuongeza manufaa zaidi kwenye uchumi wa Tanzania.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuvutia wawekezaji ambayo wamekuwa ni chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Lindi na kuahidi kwamba Serikali ya Mkoa wa Lindi itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote ili wafikie malengo yao na kuchochea uchumi wa Nchi yetu.





No comments:

Post a Comment