Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA
WIZARA ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imesajili majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi 31,598 hadi kufikia Aprili 2026, huku vyeti vya ubora 128,430 vikitoa kwa shehena za bidhaa zinazoingia nchini katika jitihada za kuimarisha usalama wa bidhaa na kulinda afya za walaji.
Taarifa hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Judith Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Kapinga amesema usajili huo wa maeneo ya chakula na vipodozi umefikia asilimia 87.8 ya lengo la kusajili na kutoa vibali 36,000 kwa mwaka.
Amesema kati ya maeneo yaliyosajiliwa, maeneo 27,295 yanajihusisha na bidhaa za chakula huku maeneo 4,303 yakijihusisha na bidhaa za vipodozi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema hadi Aprili 2026, TBS imesajili bidhaa za chakula na vipodozi 2,070 sawa na asilimia 86.3 ya lengo la kusajili bidhaa 2,400 kwa mwaka.
Kati ya bidhaa hizo, bidhaa 1,406 ni za chakula na bidhaa 664 ni za vipodozi.
Kapinga amesema Serikali imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za TBS katika kanda tisa nchini pamoja na kuendelea na ujenzi wa maabara katika kanda ya kati Dodoma na kanda ya ziwa Mwanza.
Aidha, amesema maandalizi yanaendelea kumpata mkandarasi wa ujenzi wa maabara ya kanda ya kaskazini katika mkoa wa Arusha Region.
Waziri huyo amesema TBS pia inaendelea kusajili bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi pamoja na zinazoingia kutoka nje, sambamba na kufanya tathmini za viwanda, ukaguzi wa awali na ukaguzi endelevu wa bidhaa sokoni ili kuhakikisha ubora unaozingatia viwango vinavyotakiwa.
Katika ukaguzi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, Kapinga amesema hadi Aprili 2026 jumla ya vyeti vya ubora 128,430 vilitolewa sawa na asilimia 91.7 ya lengo la kutoa vyeti 140,000 kwa mwaka.
Amesema kati ya vibali hivyo, vibali 40,225 vilitolewa kwa bidhaa zilizokaguliwa nje ya nchi na vibali 88,205 vilitolewa kwa bidhaa zilizokaguliwa ndani ya Tanzania.
Pia amesema magari 50,919 yaliyotumika kutoka nje ya nchi yalikaguliwa, kiwango kinachozidi lengo la magari 50,000 kwa mwaka kwa kufikia asilimia 101.8.
Katika kuimarisha mifumo ya ubora na uongozi wa kampuni, Waziri Kapinga amesema kampuni 15 zilithibitishwa kuwa na mifumo yenye ubora wa kimenejimenti hadi Aprili 2026, sawa na asilimia 93.8 ya lengo la kuthibitisha kampuni 16 kwa mwaka.


No comments:
Post a Comment