ARUSHA
Tume ya Madini imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika usimamizi wa rasilimali za umma baada ya kupata hati safi ya ukaguzi kwa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2024/2025 sambamba na kukusanya maduhuli yaliyofikia Shilingi Trilioni 1.192, sawa na asilimia 99 ya lengo la mwaka.
Akizungumza Mei 19, 2026 mkoani Arusha wakati wa kikao kazi cha wahasibu na wachumi wa Tume, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Tume ya Madini, CPA. Idfonce Masoud, amesema hati safi hiyo imetokana na ukaguzi uliokamilika na kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwezi Machi 2026.
CPA. Masoud amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi, nidhamu ya kazi na weledi wa timu ya wahasibu na wachumi waliotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Kanuni za Kimataifa za Uandaaji wa Hesabu za Sekta ya Umma (IPSAS), hatua iliyosaidia kupunguza hoja za ukaguzi na kuimarisha uwazi wa kifedha.
Amezipongeza pia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa mchango wao mkubwa katika ukusanyaji wa maduhuli pamoja na usimamizi madhubuti wa Katibu Mtendaji wa Tume, uliowezesha kufikiwa kwa kiwango kikubwa cha mapato ya Serikali.
“Natumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana kwa juhudi mlizozifanya katika kusimamia ukusanyaji wa maduhuli hadi kufikia kiasi kilichokusanywa kufikia tarehe 15 Mei 2026,” amesema CPA. Masoud.
Aidha, amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kutumia ipasavyo mafunzo na mada zitakazowasilishwa ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa Taasisi.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Godson Kamihanda, amesema kikao kazi hicho ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto za kiutendaji na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji huduma.
Amesema majadiliano yatakayofanyika yanatarajiwa kuzaa matokeo chanya yatakayochangia maendeleo ya Tume ya Madini na Taifa kwa ujumla.















No comments:
Post a Comment