
Na Okuly Julius, OKULY BLOG ,DODOMA
Wizara ya Ujenzi imetaja vipaumbele sita vikuu itakayovitekeleza katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali itaendelea kukamilisha miradi inayoendelea sambamba na kuwekeza katika miradi mipya yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Ulega amesema kipaumbele cha kwanza ni kuendelea na ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika majiji na miji inayokua kwa kasi ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa, Pwani na Singida.
Amesema katika Jiji la Dodoma Serikali itaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye kilometa 112.3 pamoja na upanuzi wa barabara ya Dodoma–Morogoro kutoka njia mbili hadi sita.
Kipaumbele cha pili ni kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa pamoja na nchi jirani ili kuimarisha biashara na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya miradi hiyo ni barabara ya Tanga–Pangani–Makurunge inayounganisha Tanzania na Kenya, Manyovu–Kasulu–Kabingo inayounganisha Tanzania na Burundi pamoja na Matai–Kasesya inayounganisha Tanzania na Zambia.
Kwa upande wa kipaumbele cha tatu, Wizara imeeleza kuwa itaendelea kufanya ukarabati na matengenezo makubwa ya barabara kuu na za mikoa zenye changamoto ili kulinda uwekezaji wa Serikali na kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu kwa muda mrefu.
Aidha, Serikali imepanga kuanza matumizi ya Hati Fungani za Miundombinu (Infrastructure Bond) kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa barabara kuu za kiuchumi nchini.
Kipaumbele cha nne ni kuendelea kuimarisha usafiri na miundombinu ya vivuko ambapo Serikali imepanga kununua vivuko vipya vitano kwa Ukanda wa Ziwa pamoja na kuboresha huduma za usafiri katika maeneo ya Pwani ikiwemo Nyamisati–Mafia.
Katika hatua nyingine, Wizara imeweka kipaumbele cha kuwajengea uwezo wataalam na wakandarasi wa ndani kupitia mafunzo, Mfuko wa Kusaidia Wakandarasi (CAF) pamoja na kuhamasisha ubia wa kampuni za ndani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi.
Waziri Ulega amesema Serikali itaendelea pia kuwashirikisha vijana wabunifu katika kutafuta suluhisho za changamoto za miundombinu kupitia mashindano ya ubunifu na teknolojia.
Kipaumbele cha sita ni kuendelea na ujenzi wa majengo ya Serikali pamoja na nyumba za gharama nafuu kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa nyumba 144 za gharama nafuu Temeke jijini Dar es Salaam na kuanza mradi mwingine wa nyumba 144 jijini Dodoma.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Ujenzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Sh trilioni 2.56 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.


No comments:
Post a Comment