
Na Okuly Julius,OKULY BLOG, Dodoma
Wizara ya Ujenzi imeiomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 2.56 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Hamis Ulega, amesema kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 2.46 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo huku Shilingi bilioni 97.1 zikielekezwa katika matumizi ya kawaida ya Wizara na taasisi zake.
Amesema katika fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi bilioni 92.2 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni 4.89 kwa matumizi mengineyo.
“Bajeti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inajumuisha fedha za ndani kiasi cha Shilingi trilioni 1.54 na fedha za nje Shilingi bilioni 922.4,” amesema Waziri Ulega wakati akiwasilisha hotuba hiyo bungeni jijini Dodoma.
Waziri huyo amesema fedha hizo zitawezesha kuendelea kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine muhimu inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafirishaji na kuimarisha huduma za kijamii nchini.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za miundombinu.
Mpango huo wa bajeti unatarajiwa kujadiliwa na wabunge kabla ya kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji katika mwaka wa fedha 2026/27.

No comments:
Post a Comment