NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewahimiza wawekezaji na wafanyabiashara nchini kuhakikisha wanalinda haki na usalama wa watumiaji kwa kuzingatia kanuni bora za uzalishaji kuanzia ununuzi wa malighafi, usafirishaji hadi uchakataji wa bidhaa ili kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu vya ubora vinavyokidhi matakwa ya walaji.
Waziri Kapinga ameyasema hayo leo Mei 20, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi cha SBC Tanzania (PEPSI).
Aidha, amewataka wawekezaji na wafanyabiashara kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha uzalishaji wenye tija unaowanufaisha wao binafsi pamoja na Taifa kwa ujumla.
“Endeleeni kutekeleza maelekezo mnayopewa na mamlaka za usimamizi zilizowekwa pamoja na kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutoa huduma bora na kuleta maendeleo kwa wananchi,” amesema Waziri Kapinga.
Sambamba na hilo, amezitaka mamlaka zote za usimamizi nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili kurahisisha shughuli za uwekezaji na uzalishaji nchini.
Amesema ni muhimu mamlaka hizo kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wawekezaji na wafanyabiashara kutimiza matakwa ya kisheria bila vikwazo, kupitia utoaji wa elimu, ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda na biashara mbalimbali.
“Katika kutekeleza majukumu yenu hakikisheni hamuweki vikwazo kwa wawekezaji, bali mnaendelea kutoa elimu na kufanya ukaguzi ili kuona sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa ipasavyo,” amesema.
Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea kujizatiti katika kuhakikisha uwepo wa mazingira wezeshi kwa wawekezaji kupitia maboresho ya sera, maendeleo ya miundombinu pamoja na ushirikiano endelevu na sekta binafsi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, amepongeza uongozi wa SBC Tanzania Ltd kwa dhamira yao ya kupanua uwezo wa uzalishaji, kuongeza ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Wilaya ya Temeke na Taifa kwa ujumla.
Amesema uwekezaji huo unaendana na dira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani, unaozalisha ajira, kuongeza thamani ya bidhaa na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
“Mchango wa SBC Tanzania Limited katika uchumi wetu ni mkubwa kwani kampuni hiyo inachangia takribani shilingi bilioni 150 kila mwaka kupitia kodi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hali inayoiwezesha Serikali kuendelea kutoa huduma muhimu za kijamii na kuendeleza miundombinu,” ameeleza Waziri Kapinga.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo kwa sasa inatoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya wafanyakazi wa kudumu 1,500 sambamba na ajira nyingi zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa usambazaji, sekta ya usafirishaji pamoja na viwanda saidizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa SBC Tanzania Ltd, Ziad El Khalil, amesema upanuzi wa kiwanda hicho unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko pamoja na kuendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Amesema wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanazalisha bidhaa zilizobora na zinazokidhi matakwa ya viwango.

No comments:
Post a Comment