WIZARA YA UCHUKUZI YAOMBA TRILIONI 2.87 BAJETI YA 2026/27 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 13, 2026

WIZARA YA UCHUKUZI YAOMBA TRILIONI 2.87 BAJETI YA 2026/27



Na Okuly Julius, OKULY BLOG


Wizara ya Uchukuzi imeiomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 2.87 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta ya uchukuzi katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini.

Akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mnyaa Mbarawa amesema bajeti hiyo inafikia Shilingi 2,872,738,082,000.

Profesa Mbarawa amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 126,041,236,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi 2,746,696,846,000 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha miundombinu na huduma za uchukuzi nchini.

Amesema fedha hizo zitasaidia kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta hiyo ikiwemo reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini pamoja na huduma za usafiri wa nchi kavu.

“Wizara itaendelea kuhakikisha sekta ya uchukuzi inakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi kwa kuboresha mifumo ya usafirishaji wa watu na mizigo nchini,” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha, Waziri huyo amesema pamoja na hotuba yake, ameambatisha majedwali mbalimbali yenye taarifa na takwimu muhimu kuhusu sekta ya uchukuzi kwa ajili ya kuwapa uelewa zaidi Waheshimiwa Wabunge na wananchi.

Ameeleza kuwa majedwali hayo yameainishwa katika kitabu cha hotuba kuanzia ukurasa wa 198 hadi 247 na yanapaswa kuchukuliwa kuwa sehemu ya hotuba hiyo rasmi ya bajeti.

Wizara ya Uchukuzi imeendelea kuwa miongoni mwa wizara muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji nchini.

No comments:

Post a Comment