BAJETI YA UCHUKUZI 2026/2027 YAWEKA WAZI VIPAUMBELE 8 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 13, 2026

BAJETI YA UCHUKUZI 2026/2027 YAWEKA WAZI VIPAUMBELE 8



Na Okuly Julius, OKULY BLOG


Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imesema itaendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR, uboreshaji wa bandari, usafiri wa anga pamoja na ukarabati wa reli na meli katika mwaka wa fedha 2026/27.

Akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mnyaa Mbarawa amesema Wizara imeandaa mpango na bajeti hiyo kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV 2026/27–2030/31), Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2026/27 pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano.

Profesa Mbarawa amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27, Wizara imeweka vipaumbele vinane vitakavyoongoza utekelezaji wa shughuli zake ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji nchini.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR, kuendelea na ukarabati na uboreshaji wa reli za MGR na TAZARA, pamoja na kuboresha miundombinu na huduma katika bandari mbalimbali nchini.

Vipaumbele vingine ni kuendelea na uboreshaji wa usafiri wa anga, kuendelea na ujenzi na ukarabati wa meli, kuboresha huduma za hali ya hewa, kuimarisha udhibiti, ubora na usalama wa huduma za uchukuzi pamoja na kuendelea kuboresha vyuo vya mafunzo vya kisekta.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) imetengewa jumla ya Shilingi trilioni 2.872 kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 126.04 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 4.38 ya bajeti yote, huku Shilingi trilioni 2.746 zikielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na asilimia 95.62 ya bajeti hiyo.

Profesa Mbarawa amesema kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi bilioni 100.135 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi huku Shilingi bilioni 25.906 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo (OC) kwa Wizara na taasisi zinazopokea ruzuku.

Aidha amesema katika fedha za miradi ya maendeleo, Shilingi trilioni 2.452 ni fedha za ndani huku Shilingi bilioni 294.184 zikiwa ni fedha za nje.

No comments:

Post a Comment