SEKTA YA UCHUKUZI YANG’ARA KWA MAFANIKIO 2025/26 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 13, 2026

SEKTA YA UCHUKUZI YANG’ARA KWA MAFANIKIO 2025/26



Na Okuly Julius, OKULY BLOG


Serikali imesema sekta ya uchukuzi imepata mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha 2025/26, yakiwemo ongezeko la abiria wa SGR kufikia takriban milioni 3 kwa mwaka, mapato ya ATCL kukua hadi Shilingi bilioni 626.5 kutoka Shilingi bilioni 175.69, pamoja na ongezeko la shehena bandarini kufikia tani milioni 27.83, sawa na ongezeko la asilimia 29.83.

Akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mnyaa Mbarawa amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya miundombinu ya reli, bandari, usafiri wa anga na huduma za majini.

Amesema katika usafiri wa reli ya SGR, wastani wa abiria 280,000 husafiri kila mwezi kati ya Dar es Salaam na Dodoma, sawa na abiria 9,300 kwa siku, huku mapato ya jumla ya Shilingi bilioni 169.37 yakiwa yamekusanywa tangu kuanza kwa huduma hiyo Juni 2024.

Profesa Mbarawa amesema Serikali pia ilianza rasmi usafirishaji wa mizigo kupitia SGR mwezi Julai 2025 kati ya Dar es Salaam na Dodoma (Ihumwa), hatua inayosaidia kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa nchini.

Katika hatua nyingine, amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanikiwa kuanza kujitegemea kwa kulipa mishahara na matumizi mengineyo (OC) bila ruzuku ya Serikali kuanzia Januari 2026, jambo lililoiwezesha Serikali kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 12.92 kwa mwaka.

Kuhusu bandari, Serikali inaendelea kupanua Bandari ya Dar es Salaam kupitia mradi wa Kurasini Port Extension, wenye uwezo wa kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka, huku shehena iliyohudumiwa ikiongezeka kwa asilimia 29.83 na kufikia tani milioni 27.83.

Katika usafiri wa majini, Serikali imekamilisha ujenzi wa MV New Mwanza, ukarabati wa MT Sangara, pamoja na meli nne za mizigo katika Ziwa Tanganyika zenye uwezo wa kubeba tani 8,000.

Kwa upande wa anga, ATCL imeongeza vituo vya huduma hadi 33 kutoka 23 mwaka 2020/21, huku mapato yakipanda hadi Shilingi bilioni 626.5 kutoka Shilingi bilioni 175.69, ongezeko linalozidi asilimia 250.

Aidha, Serikali imekamilisha ukarabati wa viwanja vya ndege vya Sumbawanga, Songea, Shinyanga na Tabora, pamoja na kuboresha jengo la mizigo ya haraka (perishables) katika Kiwanja cha Ndege cha KIA.

Katika hatua ya kihistoria, Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) imeanza rasmi mafunzo ya urubani mwezi Julai 2025, ambapo wanafunzi 22 tayari wamedahiliwa, hatua inayolenga kupunguza gharama za mafunzo ya marubani nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment