ASKARI 08 WATUNUKIWA TUZO KWA UTEKELEZAJI BORA WA MAJUKUMU DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 5, 2026

ASKARI 08 WATUNUKIWA TUZO KWA UTEKELEZAJI BORA WA MAJUKUMU DODOMA


Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa tuzo na zawadi kwa wakaguzi na askari 08 waliobainika kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao na kuhamasisha utendaji wenye weledi ndani ya Jeshi hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Juni 5, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gallus Hyera, aliwapongeza askari hao kwa kuonyesha kiwango cha juu cha weledi, nidhamu, uadilifu na kujituma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

ACP Hyera alisema mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha usalama na utulivu wa Mkoa wa Dodoma yanatokana na juhudi za askari wanaotekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi.

Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuboresha ustawi wa askari na kuweka mazingira bora yanayowezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi.

Kamanda Hyera aliwataka askari wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu huku wakizingatia maadili ya kazi na kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii ambayo yanaweza kuathiri taswira ya Jeshi la Polisi na utendaji wao wa kazi.

"Endeleeni kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Jeshi la Polisi. Tuzo hizi ziwe chachu ya kuongeza ari ya kazi na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi," alisema ACP Hyera.

Aliongeza kuwa askari waliofanya vizuri katika Mkoa wa Dodoma ni wengi, hivyo tuzo hizo zinawakilisha jitihada za askari wote wanaotekeleza majukumu yao kwa uzalendo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Dodoma, Mrakibu wa Polisi (SP) Idrisa Haji, aliwataka askari kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wakati wote na kujenga uhusiano mzuri na jamii ili kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Zoezi la utoaji wa tuzo na zawadi kwa askari wa Jeshi la Polisi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wao katika utekelezaji wa majukumu, kuhamasisha utendaji bora na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.






No comments:

Post a Comment