WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa haki kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha huduma za Serikali zinatolewa kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Amesema hayo leo Ijumaa, Juni 5, 2026 alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa katika viwanja vya Isimani tarafani.
Dkt. Mwigulu amesema haki za wananchi hazipaswi kucheleweshwa wala kunyimwa kwa sababu yoyote na kusisitiza kuwa kila anayestahili haki yake anapaswa kuipata kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
“Haki si hisani. Tunataka anayestahili haki apewe haki yake. Serikali haitavumilia vitendo vya kupora au kuchelewesha haki za wananchi kwa sababu yoyote ile,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa nafasi walizonazo ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na kwamba huduma zinazoweza kutolewa kwa siku hiyo zinapaswa kutolewa bila kuwazungusha wananchi.
“Linaloweza kufanyika leo lifanyike leo. Wananchi wanapofika katika ofisi za umma wanapaswa kuhudumiwa kwa heshima, haraka na kwa ufanisi,” amesema.
Pia amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi watakaobainika kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hususan wale wanaokwaza utoaji wa huduma na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Waziri Mkuu amesema uwajibikaji, uadilifu na utoaji wa huduma bora ni msingi muhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote.
Kadhalika, amewahakikishia wananchi wa Isimani kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na miradi ya maendeleo iliyopo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.








No comments:
Post a Comment