AWESO: BWAWA LA FARKWA NI UFUMBUZI WA KUDUMU WA CHANGAMOTO YA MAJI DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, June 28, 2026

AWESO: BWAWA LA FARKWA NI UFUMBUZI WA KUDUMU WA CHANGAMOTO YA MAJI DODOMA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Chemba


Serikali imesema ujenzi wa Bwawa la Farkwa ni mradi wa kimkakati utakaotoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani, huku ukifungua fursa za maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa bwawa hilo iliyofanyika katika Kijiji cha Bubutole, Kata ya Farkwa, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi ili kuwanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

Alisema bwawa hilo litakuwa na manufaa makubwa si kwa wananchi wa Chemba pekee, bali pia kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo mengine yanayozunguka, huku likiwa chanzo muhimu cha maji kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

"Mradi huu ni uwekezaji mkubwa wa Serikali unaolenga kumaliza changamoto ya maji kwa muda mrefu. Pia utatoa fursa kwa sekta ya kilimo kutumia maji ya bwawa kwa umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mazao," alisema Aweso.


Alisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wakandarasi kuhakikisha wananchi wa Chemba wanapewa kipaumbele katika ajira za kazi mbalimbali zikiwemo upishi, udereva na huduma nyingine ili wawe sehemu ya wanufaika wa moja kwa moja wa mradi huo.

Aidha, aliwataka watumishi wa Wizara ya Maji kuongeza uwajibikaji na kuwahudumia wananchi kwa wakati, akisisitiza kuwa hakuna nafasi kwa watumishi wazembe katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Waziri Aweso, bwawa hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 390 za maji, hatua itakayosaidia kuimarisha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma J. Waziri, alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa kuu lenye urefu wa mita 1,300 na kimo cha mita 32, pamoja na bwawa dogo lenye urefu wa mita 1,600 na kimo cha mita 15 litakalosaidia kuzuia upotevu wa maji.

Alieleza kuwa bwawa hilo litatoa mita za ujazo 7,236 za maji kwa siku kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji na mifugo, huku mtambo wa kisasa wa kutibu maji utakaojengwa ukiwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 128,000 za maji safi kwa siku.

Mbali na kuimarisha huduma ya maji, alisema mradi huo utafungua fursa za ufugaji wa samaki, kuongeza usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi wa eneo hilo.

Ujenzi wa bwawa unatekelezwa na kampuni ya China Jiangxi International kwa kipindi cha miezi 22.

Sambamba na utekelezaji wa mradi huo, Serikali inaendelea kuandaa makazi mapya kwa wananchi watakaoathiriwa kwa kupima viwanja katika Kijiji cha Sankwalito, kujenga shule ya msingi, nyumba za walimu, zahanati, pamoja na kuweka huduma za maji, umeme, mawasiliano na kuboresha miundombinu ya barabara.

Naye Mbunge wa Jimbo la Chemba, Mhe. Kunti Majala, alisema ujenzi wa Bwawa la Farkwa ni ndoto ambayo wananchi wa eneo hilo wameisubiri kwa miaka mingi.

Alisema mradi huo umekuwa miongoni mwa ajenda alizokuwa akizifikisha mara kwa mara bungeni kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Chemba na Dodoma kwa ujumla.

"Leo ni siku ya kihistoria kwa wananchi wa Farkwa, Chemba na Dodoma kwa ujumla. Tunamshukuru Rais na Serikali kwa kutimiza ahadi hii ya muda mrefu," alisema Majala.

Hata hivyo, aliiomba Wizara ya Maji kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa na wananchi wanaopisha mradi huo wanalipwa stahiki zao kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji wa utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment