SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA ELIMU YA JUU KUJENGA UCHUMI SHINDANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, June 28, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA ELIMU YA JUU KUJENGA UCHUMI SHINDANI

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (mbele kushoto) na viongozi wa Mkoa na Taasisi ya TIA, Mkoani Singida wakipiga makofi wakati wa kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Taaluma, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) akiwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Taaluma, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.
Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na viongozi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) baada ya kuweka jiwe la Msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63.
Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akipokea taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. Jehovaness Aikael, baada ya kuweka jiwe la Msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63, katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TIA, Prof. William Pallangyo.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Pallangyo, kukagua Jengo la Taaluma la Taasisi hiyo lililokamilika kwa asilimia 63, kabla ya kuwekwa jiwe la msingi na Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, kabla ya hafla ya kuwekwa jiwe la msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Mhe. Grace Mkoma, kabla ya hafla ya kuwekwa jiwe la msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. Jehovaness Aikael na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TIA, Prof. William Pallangyo kabla ya kuwekwa jiwe la Msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63.

Na. Peter Haule, Singida.

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, kuongeza ushindani wa uchumi na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Taaluma la Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida, chini ya Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Vyuo vya Elimu ya Juu (HEET), ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Mhe. Munde alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeifanya elimu kuwa sekta ya kimkakati katika kujenga uchumi wa kisasa unaoweza kushindana kimataifa.

“Uwekezaji unaoendelea katika vyuo vya elimu ya juu, Serikali inalenga kuongeza upatikanaji wa elimu bora, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia pamoja na kuzalisha wataalamu watakaotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo”, alisema Mhe. Munde.

Alieleza kuwa, Mradi wa HEET ni mfano wa uwekezaji unaolenga kuimarisha rasilimali watu, kuongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania kwa muda mrefu.

"Kila shilingi inayowekezwa katika elimu ni uwekezaji unaorudisha faida kupitia ongezeko la ujuzi, ajira, uzalishaji na mapato ya Taifa," alisisitiza Mhe. Munde.

Aidha, alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaiwezesha Kampasi ya TIA Singida kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha utoaji wa mafunzo katika fani za uhasibu, fedha na biashara.

Aliongeza kusema kuwa, mradi huo pia utachochea shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Singida kupitia ajira, biashara na huduma mbalimbali zitakazozunguka Kampasi hiyo.

Kadhalika, alisema kuwa, Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha rasilimali za fedha zinazopatikana kupitia ushirikiano na washirika wa maendeleo zinaelekezwa katika miradi inayochochea ukuaji wa uchumi ili kuleta tija kwa wananchi.

Kuhusu usimamizi wa fedha za umma, Naibu Waziri alisisitiza kuwa Serikali inatarajia mradi huo kukamilika kwa wakati, kuzingatia viwango vya ubora, kutekelezwa ndani ya gharama zilizoidhinishwa na kutoa thamani halisi ya fedha.

Alimtaka Mkandarasi, Mshauri elekezi na wasimamizi wa mradi kuzingatia masharti ya mkataba, kuhakikisha ubora wa kazi, kutumia nguvu kazi ya ndani pale inapowezekana pamoja na kulinda usalama wa wafanyakazi na mazingira.

Vilevile, aliutaka uongozi wa TIA kusimamia ipasavyo miundombinu hiyo baada ya kukamilika ili idumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bora za elimu, sambamba na kuandaa wahitimu wenye maadili, ubunifu na ujuzi unaokidhi mahitaji ya uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri Mhe. Munde, aliipongeza Serikali, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, uongozi wa TIA, washirika wa maendeleo, mkandarasi na wadau wote waliofanikisha hatua hiyo muhimu, huku akiahidi kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi inatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. Jehovaness Aikael na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TIA, Prof. William Pallangyo, waliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kufanikisha ujenzi wa jengo hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 63.

Alisema kuwa kukamika kwa jengo hilo kutaifanya Kampasi hiyo kuongeza Wanafunzi kutoka 2600 hadi zaidi ya 5000, jambo litakalotoa fursa zaidi kwa vijana kutoka Mkoa huo na maeneo mengine ya nchi kupata elimu.

Walisema Kampasi ya Singida ni ya muda mrefu katika kuanzishwa kwake toka mwaka 1974 ikitanguliwa na Kampasi ya Dar es Salaam, hivyo ni muda mwafaka wa Kampasi hiyo kujiimarisha kwa miundombinu ili kuweka mazingira bora zaidi ya wanafunzi kupata elimu.

Aidha waliiomba Serikali kuendelea kuongeza miundombinu ya mabweni ili kukidhi idadi kubwa ya Wanafunzi waliopo na wanaotarajiwa kuongezeka baada ya Jengo hilo kukamilika kwa kuwa kwa sasa wengi wanaishi nje ya Chuo hicho.

No comments:

Post a Comment