BIDHAA ZA SHILINGI MILIONI 394 ZATEKETEZWA MKURANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 23, 2026

BIDHAA ZA SHILINGI MILIONI 394 ZATEKETEZWA MKURANGA

NA EMMANUEL MBATILO, PWANI

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati limeteketeza tani 110 za bidhaa hafifu na zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 394 katika zoezi lililofanyika Juni 22, 2026, Mkuranga mkoani Pwani.

Bidhaa zilizoteketezwa zinajumuisha tani 26 za bidhaa za mitumba, ikiwemo nguo za ndani na taulo ambazo kwa mujibu wa viwango na sheria za nchi haziruhusiwi kuingizwa nchini kutokana na hatari zake kwa afya ya jamii.

Bidhaa nyingine zilizoharibiwa ni tani 8 za vipodozi vilivyopigwa marufuku, tani 3 za bidhaa za chakula zilizokwisha muda wa matumizi pamoja na kiasi cha bidhaa za rangi ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango vya ubora.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo, Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Bi. Noor Meghji, alisema bidhaa hizo zilipatikana kupitia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na shirika hilo katika masoko na maeneo mbalimbali ya biashara.

Alisema katika baadhi ya maeneo walibaini uwepo wa bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi na kuwaagiza wahusika kuziondoa sokoni na kuziteketeza ili kulinda afya za watumiaji.

Bi. Meghji amewataka wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa mbalimbali kwa kuhakikisha wanasoma taarifa zote muhimu zilizopo kwenye vifungashio kabla ya kufanya matumizi.

“Iwapo mtumiaji atagundua tofauti yoyote kwenye bidhaa au kipodozi anachotumia, ni muhimu kutoa taarifa kwa TBS mapema ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” alisema.

Aidha, alifafanua kuwa lengo la TBS si kuwaadhibu au kuwaumiza wafanyabiashara kwa kuharibu bidhaa zao, bali ni kuhakikisha sheria na viwango vinazingatiwa kwa manufaa ya umma. Alisema shirika hilo linaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu bidhaa zilizopigwa marufuku na zile zenye viambata hatarishi.

Wakati huohuo, TBS imetoa onyo kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora au zinazohatarisha afya ya watumiaji, ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria kwa makusudi.

Shirika hilo limeeleza kuwa wahusika wanaobainika kuingiza au kuuza bidhaa hizo wanaweza kulazimika kugharamia zoezi la uteketezaji pamoja na kukabiliwa na hatua nyingine za kisheria kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

TBS imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa au kuingizwa nchini zinazingatia viwango husika kwa lengo la kulinda afya ya wananchi, mazingira ya biashara na uchumi wa Taifa.

Bi. Meghji alisema kuwa endapo bidhaa hizo zingeendelea kusambazwa na kutumika sokoni, zingeweza kusababisha madhara makubwa kwa afya za watumiaji na kuathiri ustawi wa uchumi wa nchi.

“Tunawaasa wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa ambazo hazikidhi matakwa ya viwango, vipodozi vilivyozuiliwa pamoja na bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi. Wakaguzi wetu wanaendelea kufanya kazi muda wote na tunashirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya dola kuhakikisha bidhaa zote zinazopatikana sokoni zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment