
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika mkoani Dodoma katika Viwanja vya Chinangali kuanzia Juni 16 hadi Juni 23, 2026.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu inayosema ‘Kuchochea uwajibikaji jumuishi kwa huduma endelevu’ yalifunguliwa rasmi Jumanne Juni 17, 2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Akifungua maonesho hayo, Mhe. Kikwete alisema maonesho hayo yatumike kama eneo ambalo wananchi watapata huduma kwa urahisi, weledi na uharaka katika taasisi husika za Serikali.
Pia, ameongeza kuwa hiyo ni fursa kwa taasisi za umma kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuonesha mafanikio, ubunifu na maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa huduma kwa umma.
Wananchi wanaotembelea banda la BoT wanapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo; Uwekezaji katika hatifungani, alama za usalama katika noti, majukumu ya BoT, namna ya kupata leseni ya kutoa huduma ndogo za fedha, mfumo wa malipo wa Tanzania unavyofanya kazi na nafasi ya BoT katika uchumi wa nchi.
Ushiriki wa BoT katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuimarisha mawasiliano kwa umma, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu shughuli zake na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.





No comments:
Post a Comment