Na WMJJWM – Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kuhamasisha maendeleo na ustawi wa wananchi nchini.
Dkt. Nanauka amesema hayo leo Juni 17, 2026 wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) uliofanyika jijini Mwanza.
Amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii wana jukumu muhimu la kuhakikisha wananchi wanatambua na kutumia fursa zilizopo, kushiriki katika miradi ya maendeleo na kuachana na mila na desturi zinazokinzana na maendeleo ya jamii.
Aidha, amewataka wataalam hao kuendelea kuhamasisha malezi na makuzi ya awali ya mtoto, kuimarisha maadili mema, uzalendo na uwajibikaji wenye tija katika jamii.
Dkt. Nnauye amesema Serikali imepokea changamoto zinazowakabili Maafisa Maendeleo ya Jamii na itaendelea kushirikiana nao katika kutafuta ufumbuzi. Vilevile ameyataka mashirika mbalimbali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa maafisa Maendeleo ya Jamii, ikiwemo kutoa vitendea kazi hivyo kuwahimiza maafisa hao kuendelea kutoa huduma kwa moyo na weledi ili kuharakisha maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake rais wa CODEPATA Victor Kabuje amepongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, kwa kuendelea kusimamia na kuboresha sekta ya Maendeleo ya jamii nchini.l hivyo Wataalam hao wataendelea kutekeleza sera miongozo na kampeni mbalimbali nchini kuhakikisha jamii inakuwa na maendeleo endelevu.
Mkutano huo umehudhuriwa na wataalam wa maendeleo ya jamii kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili masuala ya kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mchango wao katika maendeleo ya Taifa.






No comments:
Post a Comment