WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUZINDUA AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 17, 2026

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUZINDUA AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA ZANZIBAR


Na Boniphace John, Dodoma


Wizara ya Katiba na Sheria inatarajia kuzindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC II) Juni 20, 2026, Zanzibar, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 17, 2026, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema kampeni hiyo itaendelea kubeba kaulimbiu isemayo: “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ikionesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa usawa, kuimarisha amani katika jamii na kuweka msingi imara wa maendeleo ya Taifa.

Dkt. Homera amesema katika awamu hiyo wananchi watapatiwa elimu, ushauri na huduma mbalimbali za kisheria zinazohusu masuala ya ndoa na talaka, mirathi na wasia, migogoro ya ardhi, haki za watoto, ukatili wa kijinsia, haki za wafanyakazi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na huduma za usajili wa matukio muhimu ya maisha na upatikanaji wa nyaraka za utambulisho.

Amesema huduma hizo zitatolewa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wadau wa sekta ya sheria kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto zao za kisheria na kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wao.

“Kampeni hii ni muhimu kwa kila mwananchi mwenye uhitaji wa msaada wa kisheria. Pia ina mchango mkubwa kwa makundi maalumu na wananchi wanaoishi maeneo ya mbali ambako upatikanaji wa huduma za kisheria bado ni changamoto,” amesema Dkt. Homera.

Ameeleza kuwa katika awamu ya pili, huduma zitatolewa kupitia mabanda yatakayowekwa katika wilaya zote za Mkoa wa Mjini Magharibi ambazo ni Wilaya ya Mjini, Magharibi A na Magharibi B.

Aidha, amesema timu ya wataalamu kutoka Wizara na taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Kamisheni ya Ardhi, Jeshi la Polisi Zanzibar, Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, Jumuiya ya Mawakili Zanzibar pamoja na taasisi za utoaji wa msaada wa kisheria na wasaidizi wa sheria, itashuka hadi ngazi ya shehia kutoa huduma mbalimbali za msaada wa kisheria.

Huduma hizo zitajumuisha utoaji wa elimu ya sheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, uandaaji wa nyaraka za kisheria na huduma nyingine muhimu zinazolenga kusogeza haki karibu zaidi na wananchi.

No comments:

Post a Comment