DKT. MWIGULU NCHEMBA ATATUA MGOGORO WA ARDHI ULIDUMU MIAKA 41 NYOLOLO MUFINDI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 6, 2026

DKT. MWIGULU NCHEMBA ATATUA MGOGORO WA ARDHI ULIDUMU MIAKA 41 NYOLOLO MUFINDI


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 41 kati ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Mtume Nyololo wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa na Familia ya Yosefa Mgavilenzi ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Michael Bakari Seveyage.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Igowole Mufindi Kusini, Waziri Mkuu alipokea malalamiko ya familia ya Yosefa Mgavilenzi kuwa eneo lake lenye ukubwa wa ekari 107 limechukuliwa na Kanisa hilo bila fidia na aliomba Waziri Mkuu amsidie ili alipwe.

Mapema wiki hii Waziri Mkuu alituma timu ya wataalamu kutoka ofisi yake ambao walikwenda katika kata ya Nyololo na kufanya vikao vya maridhiano na viongozi wa Kanisa Katoliki, familia ya Yosefa, Wazee, viongozi wa Kata ya Nyololo na kijiji cha Nyololo Shuleni walioko madarakani na wastaafu pamoja na wananchi.

Baada ya majadiliano yaliyochukuwa siku tatu pande mbili husika zilikubaliana kumaliza mgogoro kwa njia ya maridhiano ambapo Baba Askofu wa Jimbo la Mafinga, Vicent Mwagala alitoa shilingi milioni 20 kama fidia kwa familia ya Yosefa ambayo ilizipokea kwa moyo mkunjufu na kukubali kumaliza mgogoro huo.

Hati za maridhiano zilitiwa saini na Kanisa Katoliki Parokia ya Nyololo pamoja na familia ya marehemu Michael Bakari Seveyage leo Juni 5, 2026 katika kikao cha maridhiano kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Nyololo wilayani Mufindi.

Paroko wa Parokia ya Yohana Mtume Nyololo alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa sera yake ya maridhiano ambayo imemuwezesha Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kuumaliza mgogoro uliodumu kwa miaka 41.

Alimshukuru Askofu wa Jimbo la Mafinga Vicent Mwagala kwa kutoa shilingi milioni 20 kama fidia kwa mlalamikaji hatua ambayo imesaidia sana kufikia maridhiano na alisisitiza kwamba mgogoro huo umeisha na sasa wataishi kwa amani kama jamii moja.

Mchungaji John Mbwiga ambaye ni Kiongozi wa familia ya mlalamikaji aliishukuru serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba aliyetuma timu ya watalaamu kutoka ofisini kwake ambao wamemaliza mgogoro huo ulioikosesha familia amani kwa miaka mingi na kwamba sasa wataishi kwa amani.

Mwenyekiti wa Kijiji Mstaafu wa kijiji cha Nyololo Shuleni, Jeremia Mngolage alliishukuru serikali hususan Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi anayofanya ya kutatua migogoro mbalimbali katika jamii kwa njia ya mardhiano.




No comments:

Post a Comment