
Na Boniphace John, Dodoma
Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 linaloratibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Brighton Marekela, limefikia hatua muhimu baada ya washiriki 100 bora kuchaguliwa kati ya maombi 7,852 yaliyowasilishwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Washiriki hao 100 wanatarajiwa kuingia katika kambi maalum ya siku nne kwa ajili ya mafunzo na uboreshaji wa mawazo yao bunifu yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, kati ya maombi yote yaliyopokelewa, maombi 4,121 yalikidhi vigezo vya msingi vya ushiriki, ikiwemo umri unaokubalika, insha isiyozidi maneno 300 pamoja na video ya maelezo isiyozidi dakika tatu.
Washiriki waliofanikiwa kuendelea walichaguliwa kwa kuzingatia ubora wa mawazo yao, kiwango cha ubunifu, athari zinazotarajiwa katika uchumi wa Taifa na uwezekano wa kuyatekeleza kwa vitendo.
Shindano hilo linalenga kuibua na kukuza mawazo ya vijana yenye ubunifu, yanayotekelezeka na endelevu katika kulinda na kuimarisha uchumi wa Taifa dhidi ya athari za misukosuko ya kiuchumi duniani. Aidha, ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Baada ya hatua mbalimbali za tathmini, mawazo 458 yalipata alama za juu na kuwasilishwa mbele ya kamati kamili kwa ajili ya uchambuzi wa mwisho, ambapo washiriki 100 bora waliteuliwa kuingia kambini.
Washiriki hao watapata mafunzo ya kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa sekta mbalimbali pamoja na semina maalum zitakazowajengea uwezo wa kuwasilisha mawazo yao kwa ufanisi mbele ya majaji, wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, amesema baada ya mafunzo hayo washiriki watafanya mawasilisho rasmi yatakayowezesha kupatikana kwa washiriki 30 bora watakaoingia hatua ya nusu fainali na baadaye washiriki 10 bora zaidi watakaoingia katika hatua ya fainali ya mashindano hayo.
“Mshindi wa kwanza atajinyakulia shilingi milioni 50 badala ya milioni 30 zilizotangazwa awali. Mshindi wa pili atapata shilingi milioni 30, mshindi wa tatu shilingi milioni 20, huku washiriki watakaoshika nafasi ya nne hadi ya kumi kila mmoja akipata shilingi milioni tatu,” amesema Sanga.
Ameongeza kuwa washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya mashindano. Pia watapata fursa mbalimbali za kukuza na kuendeleza mawazo yao kupitia mafunzo, ushauri wa kitaalamu, mitandao ya wadau wa maendeleo na kuunganishwa na taasisi mbalimbali zitakazoweza kusaidia utekelezaji wa mawazo yao kwa manufaa binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Takwimu za uchambuzi wa maombi zinaonesha kuwa sekta ya TEHAMA na huduma za kidijitali iliongoza kwa kuvutia mawazo mengi ya ubunifu kwa asilimia 30.7, ikifuatiwa na Kilimo na Teknolojia za Kilimo (AgriTech) kwa asilimia 27.8, huku sekta ya Viwanda na Uzalishaji ikichangia asilimia 21.3.
Sekta nyingine zilizovutia mawazo ya washiriki ni Nishati na Mazingira kwa asilimia 5.8, Huduma za Kifedha (FinTech) asilimia 1.7, Usafirishaji na Mnyororo wa Ugavi asilimia 0.6, huku asilimia 12.1 zikitoka katika sekta nyingine zikiwemo utalii, afya, elimu na madini.
Awali, dirisha la kupokea mawazo bunifu lilifunguliwa Aprili 13, 2026 na kufungwa Mei 7, 2026, likiwa na kaulimbiu isemayo: “Vijana Wanafikiri, Taifa Linasonga.”
Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge chini ya Mwenyekiti wake Brighton Marekela imeeleza kuwa hata washiriki ambao hawakufanikiwa kuendelea katika hatua zinazofuata hawataachwa nyuma, kwani kuna mipango ya kutafuta njia bora za kuthamini ushiriki wao na kuwawezesha kuendelea kukuza mawazo yao ya kibunifu kwa manufaa ya Taifa.



No comments:
Post a Comment