FURSA ZA MASOMO URUSI ZAWANUFAISHA WATANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 10, 2026

FURSA ZA MASOMO URUSI ZAWANUFAISHA WATANZANIA


Na Carlos Claudio, OKULY BLOG , DODOMA 



SERIKALI imesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa elimu kwa Watanzania kupitia fursa za ufadhili wa masomo, programu za shahada za pamoja pamoja na ushirikiano wa kisayansi kati ya taasisi za elimu za nchi hizo mbili.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 10, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya elimu wakati wa ziara hiyo ya Rais Samia nchini Urusi.


Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni Chuo Kikuu cha RUDN University kumtunuku Rais Samia Shahada ya Udaktari wa Heshima pamoja na kutoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Tanzania.


“Chuo kilichomtunuku Rais shahada kimetupatia scholarship 10 tayari ili tuwe tunapeleka Watanzania kwenda kusoma kule. Tumekubaliana pia kuwa na ushirikiano mpana zaidi katika maeneo mbalimbali ya elimu na utafiti,” amesema Prof. Mkenda.


Aidha, amesema Wizara ya Elimu imefanikiwa kusaini hati tatu za makubaliano wakati wa ziara hiyo, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu katika elimu ya juu, sayansi na teknolojia kati ya Tanzania na Urusi.


Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, hati ya kwanza imehusisha wizara za elimu za nchi hizo mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa vyuo vikuu, kubadilishana walimu na wanafunzi pamoja na kukuza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na Kirusi.


Amesema hati ya pili imesainiwa kati ya Dar es Salaam Institute of Technology na MIREA – Russian Technological University ambapo wanafunzi watasoma kwa mfumo wa miaka miwili Tanzania na miaka miwili Urusi kabla ya kutunukiwa shahada zinazotambulika kimataifa.


Pia taasisi hizo zimesaini hati nyingine ya makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa programu za shahada za uzamili zitakazoendeshwa kwa ushirikiano katika nchi hizo mbili.


Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea kukamilisha makubaliano mengine yatakayorahisisha utambuzi wa vyeti na sifa za kitaaluma kwa wahitimu watakaosoma kupitia programu hizo.


“Tunataka kutumia mfumo wa Samia Scholarship kupata wanafunzi wa kwenda kusoma Urusi kwa uwazi na ushindani. Tunaamini maeneo ya sayansi, teknolojia na uhandisi ndiyo yatakayotuwezesha kunufaika zaidi na fursa hizi mpya za elimu,” amesema.

No comments:

Post a Comment