GST: MLIMA MAUTIA NI KIVUTIO KIKUBWA CHA UTALII WA JIOLOJIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 30, 2026

GST: MLIMA MAUTIA NI KIVUTIO KIKUBWA CHA UTALII WA JIOLOJIA



Na Okuly Julius,OKULY BLOG ,Kongwa - Dodoma


Katika ulimwengu unaotafuta maajabu ya asili na historia ya sayari, Tanzania imeendelea kujidhihirisha kuwa hazina ya kipekee ya utalii wa jiolojia, huku Mlima Mautia uliopo wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, ukitajwa kuwa moja ya maeneo adimu duniani yaliyowahi kuwa makazi pekee ya madini ya Yoderite — madini yanayobeba historia ya kipekee ya mabadiliko ya kijiolojia yasiyopatikana sehemu nyingine duniani.

Meneja wa Sehemu ya Jiolojia wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Maswi Solomoni, amesema Mlima Mautia ni miongoni mwa maeneo yenye thamani kubwa ya kisayansi na utalii kutokana na historia yake ya kijiolojia pamoja na ugunduzi wa madini adimu ya Yoderite.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea Mlima Mautia leo Juni 30, 2026, Solomoni alisema mlima huo ulipitia mabadiliko makubwa ya kijiolojia yaliyosababisha kutokea kwa madini hayo, ambayo kwa muda mrefu yalijulikana kupatikana Tanzania pekee.

Alisema madini ya Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1959 na mtafiti wa Marekani, Hatten Yoder, ambaye baadaye madini hayo yalipewa jina lake kama heshima kwa mchango wake katika tafiti za jiolojia.

"Baada ya kugunduliwa Tanzania mwaka 1959, madini hayo hayakupatikana sehemu nyingine yoyote duniani hadi mwaka 1998 yalipogunduliwa tena nchini Zimbabwe katika ukanda wa Zambezi Belt," alisema Solomoni.

Alieleza kuwa ugunduzi huo umeifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama nchi ya kwanza duniani kugundua madini ya Yoderite, hatua ambayo imeongeza hadhi ya taifa katika sekta ya jiolojia na utafiti wa madini.

Kwa mujibu wa Solomoni, Mlima Mautia una uwezo mkubwa wa kuwa kivutio cha utalii wa jiolojia, ambapo watafiti, wanafunzi, wanajiolojia na watalii kutoka mataifa mbalimbali wanaweza kutembelea eneo hilo kujifunza historia ya mabadiliko ya dunia kupitia miamba na madini yaliyopo.

Alisema sifa za kipekee za mabadiliko ya kijiolojia yaliyotokea katika Mlima Mautia hazijawahi kufanana na maeneo mengi duniani, jambo linaloufanya kuwa maabara ya asili kwa tafiti za kisayansi pamoja na kuongeza fursa za maendeleo ya utalii wa jiolojia nchini.

Kutokana na utajiri huo wa kipekee wa kiasili, wataalamu wanaamini kuwa uwekezaji katika uhifadhi, utafiti na utangazaji wa Mlima Mautia unaweza kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo vinavyoongoza Afrika katika utalii wa jiolojia, sambamba na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.






No comments:

Post a Comment