RAIS DKT.SAMIA S. HASSAN KUFUNGUA MKUTANO MKUBWA WA MADINI NOVEMBA 2026 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 27, 2026

RAIS DKT.SAMIA S. HASSAN KUFUNGUA MKUTANO MKUBWA WA MADINI NOVEMBA 2026


Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia S. Hassan anatarajiwa kufungua rasmi Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026) utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Akizungumza leo Juni 27, 2026 wakati wa uzinduzi wa TMIC 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema serikali imeamua kujenga uchumi wa viwanda unaotokana na madini kwa kuwekeza katika uchakataji na uyeyushaji wa madini badala ya kuendelea kuuza malighafi.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo, "Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi," inaakisi dira ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini barani Afrika.

Kwa mujibu wa Mhe. Mavunde, amesema Tanzania tayari ina viwanda vinane vya kusafisha dhahabu, huku Mkoa wa Dodoma ukiwa na viwanda tisa vinavyojengwa na vinavyoendelea na uzalishaji pamoja na kiwanda kikubwa cha kuyeyusha madini ya nikeli na shaba.

"Zaidi ya Sh bilioni 600 zinawekezwa katika ujenzi wa kiwanda cha chuma kitakachotumia asilimia 100 ya malighafi za ndani, huku uwekezaji mwingine ukiendelea Kigamboni na Tanga kwa ajili ya uchakataji wa madini ya 'Heavy Mineral Sands' na mradi wa madini ya niobium wa Panda Hill, Mbeya," amesema Mhe. Mavunde

Amesema, katika kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye sekta hiyo, thamani ya manunuzi kupitia mpango wa 'Local Content' imefikia Sh trilioni 5.1, huku bidhaa 20 zikitakiwa kuzalishwa na wazawa kwa ajili ya kuhudumia migodi mikubwa.

 Amesisitiza wafanyabiashara kuzingatia uaminifu na viwango vya kimataifa ili kunufaika zaidi na fursa hizo.

Amesema sekta ya madini imeendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi kwa kuingiza Sh trilioni 1.374 katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kiwango kilichovuka lengo la Sh trilioni 1.2 kwa mwaka huu wa fedha.

Mhe. Mavunde, amesema Serikali imeidhinisha asilimia 10 ya mapato yote ya sekta ya madini kuelekezwa kwenye utafiti wa kina wa jiofizikia ili kuongeza maeneo yanayofahamika kuwa na madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amesema Serikali inaandaa mfuko maalumu wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ambao licha ya changamoto za mitaji na teknolojia, wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaanza operesheni ya kufuta kidijitali leseni zote za madini zisizotumika. Wamiliki watakaoshindwa kuwasilisha taarifa ndani ya muda uliowekwa watapewa notisi ya siku 30 kabla ya leseni hizo kujifuta moja kwa moja.

Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha utajiri wa madini unakuwa chachu ya kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi kupitia uongezaji thamani badala ya kuishia kwenye uchimbaji pekee.

Amesema TMIC 2026 utawakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi za fedha, kampuni za madini, wataalamu wa teknolojia, watafiti na wadau wengine kutoka duniani kote kujadili fursa za uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.

 "Huu ni wakati wa kuingia katika awamu mpya ya uwekezaji, ubunifu na ukuaji wa sekta ya madini nchini," amesema.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, amesema mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 2,000 na watoa mada zaidi ya 100 kutoka mataifa zaidi ya 50, huku zaidi ya mada 20 zikijadiliwa zikiwemo sera, kodi, uwekezaji, teknolojia, nishati safi, madini ya kimkakati, uongezaji thamani na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG).

Mchwampaka amesema TMIC 2026 pia utaweka mkazo katika maendeleo ya wachimbaji wadogo pamoja na ushirikishwaji wa wanawake na watu wenye ulemavu katika mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini. Mkutano huo unatarajiwa kufungwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

No comments:

Post a Comment