UDOM YAONESHA BUNIFU ZA KIDIJITALI KUCHOCHEA DIRA YA TAIFA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 27, 2026

UDOM YAONESHA BUNIFU ZA KIDIJITALI KUCHOCHEA DIRA YA TAIFA 2050


Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE), kimehitimisha Wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa kuwasilisha bunifu na tafiti za kidijitali zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali za jamii na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.


Maonesho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu isemayo, "Ubunifu wa Kidijitali kwa Tanzania 2050: Kuchochea Mabadiliko na Kuwezesha Maisha ya Watu," yakilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Akifunga rasmi maonesho hayo katika Ukumbi wa Auditorium wa Ndaki ya CIVE, Naibu Makamu Mkuu wa UDOM anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jefta Sunzu, alisema ubunifu wa kidijitali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya dunia ya sasa, huku akisisitiza kuwa vyuo vikuu vina jukumu la kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia kutatua changamoto za jamii.

Alisema UDOM itaendelea kuunga mkono tafiti na bunifu za wanafunzi na watafiti wake ili kuzalisha suluhisho endelevu, kukuza uchumi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa Tanzania katika nyanja za sayansi, teknolojia na ubunifu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti, Machapisho na Ushauri Elekezi wa UDOM, Prof. Placidius Ndibalema, alisema chuo kitaendelea kuwekeza katika tafiti na ubunifu unaolenga kutoa majibu ya changamoto za maendeleo ya Taifa na kuongeza mchango wa elimu ya juu katika ukuaji wa uchumi.

Naye, Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE), Dkt. Hector Mon, aliwapongeza wanafunzi kwa bunifu walizoonesha na kuwataka kuendelea kuzingatia mafunzo ya vitendo ili kujenga uwezo wa kushindana katika soko la ajira na kubuni teknolojia zinazokidhi mahitaji ya jamii.

Katika maonesho hayo, wanafunzi na wahadhiri waliwasilisha mifumo mbalimbali ya kidijitali, programu za kompyuta na tafiti za kisayansi zinazolenga kuboresha sekta za elimu, afya, kilimo, usafirishaji, biashara na mazingira, zikionesha mchango wa UDOM katika kukuza ubunifu na maendeleo ya Taifa.


No comments:

Post a Comment