SERIKALI YAENDELEA KUCHUKUA HATUA KUIMARISHA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII KWA WATOTO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 26, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUCHUKUA HATUA KUIMARISHA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII KWA WATOTO.



Na Jackline Minja, WMJWM Dodoma


Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha ustawi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuratibu vikao shirikishi vya kijamii vinavyowapa elimu wazazi na walezi kuhusu wajibu wao wa malezi, matunzo na ulinzi wa watoto, hususan yatima na watoto wenye ulemavu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Bungeni jijini Dodoma leo, Juni 26, 2026, alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka wazazi kutoruhusu migogoro yao ya kifamilia kuwa chanzo cha watoto kukosa malezi na kuishia kuishi mitaani katika mazingira hatarishi.

"Wazazi niwasihi pale ambapo migogoro ya wazazi itakuwa imefikia hatua ya kushindwa kuwalea watoto kwa wakati, ni vyema mkakawapeleka watoto hao katika vituo vya ustawi wa jamii ili wapate malezi na ulinzi stahiki kwa muda, badala ya kuwaacha wakitelekezwa." amesema Dkt. Gwajima

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Msalala, Mhe. Mabula Johnson Magangila Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Mei 2026, jumla ya wazazi na walezi 469,634 walifikiwa kupitia elimu hiyo, wakiwemo wanaume 178,343 na wanawake 288,025, huku watu wenye ulemavu waliofikiwa wakiwa 3,266 lengo ni kuwajengea uwezo wazazi na walezi ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na ulinzi stahiki ndani ya familia na jamii.

"Utoaji wa elimu hii ni endelevu na unafanyika kupitia programu na kampeni mbalimbali za Serikali, ikiwemo kampeni ya "Familia Bora, Taifa Imara", inayolenga kuimarisha malezi bora, mshikamano wa familia na ustawi wa watoto nchini."amesema Mhe. Mahundi

Aidha Mhe. Mahundi amesisitiza kuwa ushiriki wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ni nguzo muhimu katika kuhakikisha watoto wote, hususan walio katika mazingira magumu, wanapata haki zao za msingi, ulinzi na fursa za kukua katika mazingira salama yatakayowajengea maisha bora ya baadaye.

No comments:

Post a Comment