TAEC YAENDESHA MAFUNZO YA UTAYARI DHIDI YA DHARURA ZA KEMIKALI, KIBAIOLOJIA, KIRADIOLOJIA NA KINYUKLIA (CBRN) ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 23, 2026

TAEC YAENDESHA MAFUNZO YA UTAYARI DHIDI YA DHARURA ZA KEMIKALI, KIBAIOLOJIA, KIRADIOLOJIA NA KINYUKLIA (CBRN) ZANZIBAR


Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendesha mafunzo maalum ya siku nne kuhusu utayari na mwitikio wa dharura za Kemikali, Kibaiolojia, Kiradiolojia na Kinyuklia (CBRN) yanayofanyika Zanzibar. Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki 25 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na wadau washirika.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika katika Ofisi za TAEC Zanzibar, Dunga Zuze, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha uwezo na utayari wa wataalamu katika kushughulikia hatari zinazotokana na kemikali, vimelea vya kibayolojia, mionzi na nyuklia ili kuhakikisha usalama wa wananchi pamoja na ulinzi wa mazingira.

Prof. Mohammed ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TAEC za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa majanga na matukio ya dharura nchini.

Washiriki wa mafunzo hayo wanatoka katika taasisi mbalimbali zikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya SMZ, Wizara ya Afya, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Zanzibar, Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo Zanzibar pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Dkt. Remigius Kawala, amesema mafanikio ya mafunzo hayo yatachangia kujenga mazingira salama zaidi kwa jamii na kuhakikisha uwepo wa mwitikio madhubuti wakati wa matukio hatarishi yanayohusisha nyuklia, mionzi, kemikali na vimelea vya kibayolojia.

Ameongeza kuwa mafunzo ya utayari ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa taasisi mbalimbali kukabiliana na hatari za CBRN zinazoweza kujitokeza wakati wowote, hivyo kuwa sehemu muhimu ya maandalizi na usimamizi wa majanga.

Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kusini Unguja, Ali Hamad Said, amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuimarisha utendaji wao wa kazi za kila siku kwa kuwa yamewakutanisha wadau muhimu wanaoshiriki katika kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Usalama wa Chakula wa Zanzibar Food and Drug Agency (ZFDA), Dkt. Khamis Ali Omary, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha usalama wa chakula na kwamba chakula kinaweza kutumika kama njia ya kusambaza vihatarishi mbalimbali, hivyo mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka katika kujenga uwezo wa wataalamu na kuimarisha mifumo ya udhibiti kwa manufaa ya umma.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Bi. Jabu Sharifu Haji, ameishukuru TAEC kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa kutokana na Zanzibar kuwa eneo la visiwa, ni muhimu kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na majanga na dharura za aina mbalimbali ili kulinda maisha ya wananchi na mazingira.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa, ushirikiano na uwezo wa taasisi husika katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na matukio ya CBRN kwa ufanisi zaidi.

No comments:

Post a Comment