TARURA YAMALIZA CHANGAMOTO YA BARABARA KATA YA NANYANGA, WILAYANI TANDAHIMBA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 30, 2026

TARURA YAMALIZA CHANGAMOTO YA BARABARA KATA YA NANYANGA, WILAYANI TANDAHIMBA.



Na Mwandishi Wetu, Tandahimba - Mtwara


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa RISE, program ya uondoaji vikwazo vya barabara (Bottleneck) imekamilisha ujenzi wa kalavati sambamba na matengenezo ya barabara ya Mwindi - Mnauke yenye urefu wa kilomita 8 katika Kata ya Nanyanga wilayani Tandahimba, mkoa wa Mtwara.

Kukamilika kwa mradi huo kumeondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika Kata hiyo na vijiji vya Miule, Nanyanga na Milongodi ambavyo ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho katika wilaya ya Tandahimba.

Wakizungumza na Maafisa kutoka Kitengo cha Habari cha TARURA wakati wa ziara maalum ya kutembelea miradi ya RISE inayofadhiliwa na Benki ya Dunia wananchi wa Kata hiyo wameishukuru Serikali Kwa kuwaondolea adha kubwa ya ubovu wa miundombinu ya barabara waliyokumbana nayo kwa muda mrefu.

Bi. Salma Mwaya, mkazi wa Kijiji cha Mnauke kata ya Nanyanga amesema kabla ya ujio wa mradi huo hali ya barabara haikuwa nzuri kwa jinsi walivyokuwa wanapata shida.

"Maji yakijaa tulikuwa tunapata shida sana jinsi ya kuvuka iwe kwa miguu au hata kwa baiskeli, yaani hali ilikuwa ngumu. Wakazi wa Mwindi wanaoenda Nanyanga kupata huduma za mahitaji ya kila siku kama vile madukani na huduma nyingine za kijamii walikuwa wanapata shida sana." Amesema Salma.

Kwa upande wake Bw. Mustapha Ismail Chilumba mkazi wa Mnauke amesema kabla ya ujenzi wa daraja na barabara ilifikia hatua watu wenye mizigo walikuwa wanavushwa kwa pesa kuanzia shilingi 2000 hadi 5000 inategemea na ukubwa wa mzigo uliobeba.

Kwa mujibu wa Bw. Chilumba, baada ya mavuno ya korosho wananchi wa Kijiji chao walikuwa wanasafirisha mazao yao kwa kuzunguka kupitia vijiji vya Malamba na Miule ili yaweze kufika ghalani na kuongeza kuwa mpaka kufika hatua hiyo wanaishukuru sana serikali kwani imewasaidia vya kutosha kutokana na hali ngumu iliyokuwepo awali.

Akielezea umuhimu wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tandahimba Mhandisi Innocent Ambrosi amesema eneo lililotekelezwa mradi lilikuwa hailipitiki kabisa wakati wa masika na hata wakati wa kiangazi.

Mhandisi Ambrosi amebainisha kuwa baada ya kujenga daraja na barabara hii kumekuwa na unafuu mkubwa wa usafiri na usafirishaji kwa vijiji vya Mnauke na Mwindi na kuongeza kuwa vijiji vyote ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho ambalo ni zao la kiuchumi kwenye Wilaya yao ya Tandahimba na ameishukuru serikali kupitia mradi wa RISE kwa ujenzi wa daraja na barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment