TARURA YANOA WATAALAMU KUSIMAMIA VIKUNDI VYA KIJAMII VYA MATENGENEZO YA BARABARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 15, 2026

TARURA YANOA WATAALAMU KUSIMAMIA VIKUNDI VYA KIJAMII VYA MATENGENEZO YA BARABARA


‎Na Mwandishi Wetu - Arusha

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mwaka wa pili wa Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (Community Based Routine Maintenance - CBRM) kwa kuwajengea uwezo wataalamu wake kutoka mikoa sita nchini.
‎Mafunzo hayo ya siku sita yanayofanyika jijini Arusha kuanzia Juni 15 hadi 21, 2026, yanawakutanisha wataalamu kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Manyara, Iringa na Singida kwa lengo la kuwapa ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao.
‎Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa Programu ya CBRM, Mhandisi Richard Misa amesema kuwa mpango huo unalenga kuimarisha matengenezo ya barabara za vijijini na mijini huku ukitoa fursa za ajira na kipato kwa wananchi kupitia vikundi vya kijamii vitakavyoshiriki katika shughuli za matengenezo ya kawaida ya barabara.
‎Amesema mafunzo hayo yameandaliwa na TARURA kwa kushirikiana na wataalamu washauri kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) huku yakijikita katika miongozo na taratibu za ununuzi pamoja na usimamizi wa mikataba ya vikundi vya kijamii vitakavyotekeleza kazi za matengenezo ya barabara katika mwaka wa fedha 2026/27.
‎Kwa mujibu wa Mhandisi Misa, washiriki pia wanapatiwa mafunzo kuhusu miongozo ya uundaji wa vikundi vya kijamii, usimamizi wa utekelezaji wa kazi na mbinu za kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi huku vikichangia kuboresha hali ya miundombinu ya barabara.
‎Washiriki wa mafunzo hayo ni Wahandisi pamoja na Wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka TARURA Makao Makuu, Mikoa na Wilaya sambamba na wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi za Wakurugenzi wa Wilaya.
‎TARURA inaendelea kutekeleza Mpango wa CBRM kupitia mradi wa RISE kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri vijijini na mijini huku ikihamasisha ushiriki wa jamii katika utunzaji wa miundombinu ya barabara na kuongeza ajira kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment