Na Carlos Claudio, Dodoma.
Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kufanya mkutano maalum wa kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma kuanzia Juni 15 hadi Julai 3, 2026 katika Jiji la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utoaji wa haki na uwazi katika utumishi wa umma nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma zilizopo Chimwaga Hall jijini Dodoma, Kaimu Katibu wa Tume hiyo, John Mbiso amesema mkutano huo wa nne kwa mwaka wa fedha 2025/2026 utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Mwanza.
Mbiso amesema Tume imepewa mamlaka ya kupokea na kushughulikia rufaa pamoja na malalamiko ya watumishi wa umma wasioridhishwa na maamuzi yaliyotolewa dhidi yao kwa mujibu wa kifungu cha 12(1)(d) kikisomwa pamoja na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 Marejeo ya mwaka 2023.
Amesema katika mkutano huo, Tume itajadili na kutoa maamuzi kuhusu rufaa na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na watumishi wa umma kutoka maeneo tofauti nchini.
Aidha, amesema warufani na warufaniwa walioomba kufika mbele ya Tume watapatiwa nafasi ya kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022.
Mbali na kusikiliza rufaa na malalamiko, Tume pia itapitia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika hatua nyingine, Tume hiyo itafanya ziara katika baadhi ya taasisi za serikali zilizopo jijini Mwanza kwa lengo la kutoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira pamoja na mamlaka za nidhamu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi wa rasilimali watu serikalini.
Sambamba na hilo, watumishi wa umma katika taasisi hizo watapatiwa elimu kuhusu haki na wajibu wao ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Tume ya Utumishi wa Umma imeeleza kuwa itaendelea kusimamia misingi ya haki, uwazi na usawa katika utumishi wa umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
..




No comments:
Post a Comment