CBE YAIMARISHA MAFUNZO YA FEDHA NA TEHAMA KUPITIA MABORESHO YA MITAALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 10, 2026

CBE YAIMARISHA MAFUNZO YA FEDHA NA TEHAMA KUPITIA MABORESHO YA MITAALA

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kipo katika mchakato wa kupitia na kuhuisha mitaala tisa ya masomo ili iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), pamoja na mahitaji ya sasa ya soko la ajira nchini.

Akizungumza Juni 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wadau uliowakutanisha zaidi ya taasisi 40, Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Tandi Lwoga, amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha chuo kinazalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.

Prof. Lwoga amesema hatua hiyo pia inalenga kukiandaa chuo kuwapokea wanafunzi wanaotoka katika mfumo mpya wa elimu ya sekondari unaosisitiza zaidi amali na umahiri, hivyo kuhitaji mitaala inayozingatia maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sekta mbalimbali za uchumi.

Mkutano huo ulihusisha wanataaluma kutoka vyuo mbalimbali, wawakilishi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), wawakilishi wa shule za sekondari pamoja na wadau wa elimu kutoka sekta za umma na binafsi.

Ameeleza kuwa mapitio hayo pia yanazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia.

Mitaala inayofanyiwa mapitio ni pamoja na Banking and Finance, Accounting and Finance, Accounting and Taxation, Digital Marketing, Business Administration, Finance and Economics, Bachelor Degree in Business Studies, Bookkeeping na Master of Science in IT Project Management.

Katika maboresho hayo, CBE imejumuisha masuala ya Akili Mnemba (AI) katika masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), huku masomo ya bima yakiongezwa katika programu za fedha ili kuimarisha uelewa wa wanafunzi kuhusu sekta hiyo inayokuwa kwa kasi.

Uongozi wa chuo umesisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau, hususan waajiri, katika mchakato wa kuandaa mitaala hiyo utasaidia kuzalisha wahitimu wenye ushindani katika soko la ajira, wenye uwezo wa kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment