UTUMISHI WA UMMA NI HUDUMA - DKT. MWIGULU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 6, 2026

UTUMISHI WA UMMA NI HUDUMA - DKT. MWIGULU


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watumishi wa umma kote nchini watambue na wathamini nafasi za kazi walizonazo kwamba ni huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi.

“Ninapokuwa kwenye hizi ziara, nimekuwa ninawaambia watumishi wenzangu walioko maofisini kwamba kuwa kwenye hizi nafasi ni huduma, ni utumishi na kuwazungusha watu wanapotaka hizo huduma ni ushamba,” alisema. 

Waziri Mkuu alitoa wito huo jana jioni (Ijumaa, Juni 05, 2026) wakati akizungumza na wakazi wa Jimbo la Isimani katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kijiji cha Isimani, Kata ya Kihorogota, Wilaya ya Iringa, Mkoani Iringa.

“Tutahakikisha hoja zote zinazotolewa na wananchi zinafanyiwa kazi kwa sababu huo ndiyo wajibu wa Serikali kuwatimizia wananchi yale yaliyo mahitaji yao ya kila siku ili waweze kufanya kazi wakiwa na utulivu. Nitoe rai kwa ofisi zote za umma, tuyazingatie hayo,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi wa umma waache kupuuza haki za wananchi na hasa katika maeneo ambayo mhimili wa mahakama unakuwa umetoa haki hizo. “Kuna maeneo unakuta mahakama imetoa haki lakini baadhi ya watumishi wanakuwa na kiburi na wanapuuzia. Hili halikubaliki. Hili si ombi. Wanaokaidi nimekuja na dawa yao. Lazima tukubali kuwa mtu atapata tabasamu kama haki yake anaipata.”

Alisema baada ya kukamilisha ziara zake kwenye mikoa 10, Waziri Mkuu ataitisha kikao mubashara kwa njia ya mtandao ili kupokea taarifa ya kila mkoa jinsi ulivyotatua kero za wananchi zilizoibuliwa katika mikoa yao. “Nitataka kujua yapi yaliibuliwa, yapi yamefanyiwa kazi na yapi yamekwama na kama yamekwama ni kwa nini,” alisema.

Mpaka sasa, Waziri Mkuu amekwishazuru mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Rukwa, Katavi, baadhi ya wilaya za mikoa ya Dodoma na Singida na leo atahitimisha wilaya za mkoa wa Iringa.

Mapema, Mbunge wa Isimani, Emmanuela Mtatifikolo ambaye aliapishwa jana, aliomba jimbo hilo lipatiwe hadhi ya kuwa na Halmashauri ya Wilaya kutokana na jiografia yake ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Akitoa mfano, mbunge huyo alisema: “Baadhi ya wananchi kutoka Maperamengi wanapotaka kwenda Ihemi zilipo ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wanalazimika kupanda boti (kuvuka bwawa la Mtera) hadi Migori ili waweze kupata usafiri wa magari. Wanapita Iringa mjini kabla ya kufika huko na umbali wa safari hiyo unagharimu sh. 60,000/-.” 

Aliomba pia wajengewe vituo vya afya kwenye kata za Nyang’olo na Izazi ili viweze kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo lakini pia kuhudumu nyakati za dharura endapo kutatokea ajali katika mlima Nyang’olo.

No comments:

Post a Comment