AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMUUA BABA YAKE MZAZI NA BABA YAKE MDOGO JIJINI DAR ES SALAAM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 18, 2026

AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMUUA BABA YAKE MZAZI NA BABA YAKE MDOGO JIJINI DAR ES SALAAM



Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam



Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Hosamu Hamza Juma maarufu kama Maopena kwa tuhuma za kuwaua baba yake mzazi, Hamza Juma Omari (48) na baba yake mdogo, Ally Juma Omari (37), kisha kufukia miili yao katika shimo ndani ya eneo la nyumba yao, Mtaa wa Sindano, Mwananyamala.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 18, 2026 na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri baada ya kuonekana akiwa na kisu kilichokuwa na damu pamoja na nguo zake zilizokuwa zimechafuliwa damu.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa wakati mahojiano na mtuhumiwa yalipokuwa yakiendelea, majira ya saa 4:00 usiku Polisi wa Kituo cha Oysterbay walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kulikuwa na damu nyingi katika nyumba moja iliyopo Mtaa wa Sindano, Mwananyamala, huku watu watatu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo wakionekana kutoweka.

Baada ya uchunguzi wa awali uliohusisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi, miili ya watu wawili iligunduliwa ikiwa imefukiwa kwenye shimo ndani ya eneo la nyumba hiyo. Miili hiyo ilithibitika kuwa ni ya Hamza Juma Omari na Ally Juma Omari.

Polisi wamesema uchunguzi wa kina wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa ndiye anayehusishwa na mauaji hayo. Hata hivyo, chanzo halisi au sababu iliyomfanya kutekeleza tukio hilo bado haijabainika na inaendelea kufanyiwa uchunguzi.

Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano walioutoa, likisema taarifa walizotoa zimekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo.

Aidha, Polisi wamewahakikishia wananchi kuwa uchunguzi unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa mara utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment