
Na Mwandishi Wetu, OKULY BLOG, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda ametoa wito kwa watafiti, taasisi za utafiti, wavumbuzi na wadau wote kujisajili kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISSTI) na kuhakikisha taarifa zao zinahuishwa mara kwa mara ili kuleta maendeleo kwa njia ya sayansi na Teknolojia.

Akizungumza leo Julai 2 mwaka huu jijini Dar es salaam wakatika wa uzinduzi wa mfumo wa NISSTI, waziri wa Elimu, sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema utafiti unahitaji uhuru wa kitaaluma, lakini mafanikio yake yanategemea uratibu madhubuti na ushirikiano wa sekta zote.
Amesema sera mpya lazima iendane na mahitaji ya wakati na iwe chachu ya mageuzi ya ndoto kubwa na uthubutu katika kuchukua hatua.
"Nawaalika vijana wa Tanzania kuikumbatia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama njia ya kutatua changamoto za jamii, kuunda ajira na kuijenga Tanzania yenye uchumi shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia. Mustakabali wa Taifa letu uko mikononi mwa vijana wake." Amesema Prof. Adolf Mkenda.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH , Dkt Amos Nungu amesema maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH si ya kuangalia walipotoka badala yake ni kuangalia Tanzania ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuelekea Dira ya Taifa 2050."
"Sayansi na ubunifu lazima vionekane, vieleweke, vifikike kwa urahisi na viwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi." Amesema
Amesema anataka kila mtafiti, mbunifu na taasisi ionekane, iunganishwe na ipate fursa kupitia mfumo mmoja wa kitaifa.
Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya COSTECH Prof. John Kondoro amesema Kamisheni ya COSTECH itaendelea kuisimamia Tume kwa ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa weledi, kwa wakati na kwa matokeo yanayopimika.
Amesema taarifa zinazopatikana kupitia NISSTI zinapaswa kuwa msingi wa kupanga vipaumbele vya taifa, kuelekeza uwekezaji na kuongeza tija ya utafiti na ubunifu.
"Tunataka NISSTI uwe mfumo hai, unaoaminika na unaosaidia Tanzania kujenga uchumi wa maarifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."




No comments:
Post a Comment