PROFESA KABUDI: USAFI WA MAZINGIRA NI MSINGI WA AFYA, UCHUMI NA HAKI ZA BINADAMU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 2, 2026

PROFESA KABUDI: USAFI WA MAZINGIRA NI MSINGI WA AFYA, UCHUMI NA HAKI ZA BINADAMU






Na Okuly JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),Profesa Palamagamba Kabudi, amesema usafi na uhifadhi wa mazingira si suala la afya pekee, bali ni nguzo muhimu ya afya ya umma, ukuaji wa uchumi, maendeleo endelevu na ulinzi wa haki za binadamu.

Aidha, amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutunza mazingira kwa hiari na kuwajibika bila kusukumwa.

Akifungua Mkutano wa Pili wa Kitaifa wa Wadau wa Usafi wa Mazingira Julai 2,2026 jijini Dodoma , Profesa Kabudi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za usafi wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha afya za wananchi.

Apongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuwekeza katika miradi ya maji, afya na usafi wa mazingira, akisema hatua hizo zinaweka msingi imara wa maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Profesa Kabudi pia ameipongeza EWURA kwa kupanua wigo wa usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira na kuitaka mamlaka hiyo kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa viwango vya huduma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama.

Aidha, amewataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo, kutunza mifereji ya maji, kupanda miti na kushiriki kikamilifu katika kampeni za usafi wa mazingira huku akisisitiza kuwa maendeleo ya miji, ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa taifa haviwezi kupatikana bila mazingira safi, salama na yanayohifadhiwa ipasavyo.

Vilevile, amewataka wataalamu wa mipango miji na mamlaka husika kudhibiti ongezeko la makazi holela, kuwekeza katika miundombinu ya majitaka na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya usafi wa mazingira ili kuhakikisha huduma hizo zinakuwa endelevu na zinawafikia wananchi wote.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. Kunti Majala , amesema changamoto za mazingira zinaendelea kuchangia vifo vinavyoweza kuzuilika, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu kwa umma pamoja na usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira.




Naye Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe, amesema bado kuna pengo kubwa la kitaasisi katika usimamizi wa majitaka, akibainisha kuwa mamlaka 24 pekee kati ya 84 nchini ndizo zenye mipango ya matibabu ya majitaka na tope la kinyesi.

Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mwongozo mpya wa usimamizi wa mazingira uliozinduliwa wakati wa kongamano hilo.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri, amesema kasi ya ukuaji wa mji wa Dodoma inahitaji uwekezaji zaidi katika miundombinu ya usafi wa mazingira ili kuhakikisha ukuaji wa mji unaendana na huduma bora kwa wananchi.

Mkutano huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mifumo ya usafi wa mazingira nchini, kwa lengo la kujenga miji na vijiji salama, safi, yenye afya na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.







No comments:

Post a Comment