EAC YAFANIKISHA MKUTANO WA KWANZA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA MASUALA YA KIJAMII, WASAINI RIPOTI YA UTEKELEZAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 8, 2026

EAC YAFANIKISHA MKUTANO WA KWANZA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA MASUALA YA KIJAMII, WASAINI RIPOTI YA UTEKELEZAJI


Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Mawaziri wa Masuala ya Kijamii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umehitimishwa Julai 7, 2026 jijini Dar es Salaam, kwa kusainiwa kwa ripoti maalumu inayohusu uwekaji wa sera na mikakati thabiti katika sekta za jinsia, watoto, vijana, wazee, hifadhi ya jamii, kazi, ajira na uhamiaji.

Mawaziri kutoka nchi zote 8 wanachama wa EAC wameidhinisha na kusaini ripoti hiyo ili ianze kutekelezwa kikanda, ikilenga kuhakikisha kuwa faida za mtangamano wa kiuchumi na kijamii zinamfikia kila mwananchi kwa usawa, baada ya kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa na wataalamu na Makatibu Wakuu.

Mkutano huo wa kihistoria uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayeshughulikia Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda, Mhe. Rebecca Kadaga, ambaye aliongoza zoezi la utiaji saini wa ripoti hiyo kwa kushirikiana na Mawaziri wenzake wa ukanda huo.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana) Mhe. Joel Nanauka, akiambatana na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Maryprisca Mahundi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Dkt. Eveline Munisi, pamoja na Makatibu Wakuu, wataalam wa wizara husika, na wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Katika majadiliano hayo, viongozi hao walisisitiza kuwa utekelezaji wa sera hizi utaleta mageuzi makubwa na ya kihistoria katika mifumo ya ajira, ulinzi wa jamii, ustawi wa makundi maalum, pamoja na usimamizi madhubuti wa masuala ya uhamiaji katika ukanda mzima.

Kuhitimishwa kwa mkutano huo na kusainiwa kwa ripoti hii ya pamoja kunadhihirisha dhamira thabiti ya EAC katika kujenga ukanda wenye sera shirikishi, maendeleo jumuishi, na ustawi endelevu kwa wananchi wake.

No comments:

Post a Comment