FEDHA ZA MARATHON ZILETE TIJA KWA WALENGWA ~ Dkt. MWIGULU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 26, 2026

FEDHA ZA MARATHON ZILETE TIJA KWA WALENGWA ~ Dkt. MWIGULU


Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka wizara na taasisi zinazonufaika na fedha za NBC Marathon zihakikishe zinatumika kwa uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha, ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kuleta matokeo, tena matokeo yanayopimika. 

Amesisitiza kuwa kila shilingi inayowekezwa katika mbio hizo zinapaswa kuleta matokeo yanayoonekana, kwa sababu unaposhughulika na masuala ya afya, unaongelea uhai wa Watanzania.

Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa NBC Dodoma Marathon imeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya riadha kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha afya, kuimarisha ustawi wa jamii na kuchangia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Nchemba amesema hayo leo Julai 26, 2026, alipokuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa msimu wa saba wa NBC Dodoma Marathon uliofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ukiwa na kaulimbiu ya #KataWeseOkoaMaisha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu aliwapongeza Benki ya NBC, wadhamini na washiriki wote kwa kufanikisha tukio hilo na kusema Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.

"Napenda kuwapongeza waandaaji wa NBC, wadhamini na washiriki wote. Hili ni jambo jema; si la michezo pekee bali ni jukwaa la kufadhili na kuimarisha ustawi wa jamii," alisema.

Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya na kuimarisha huduma za matibabu kwa kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

"Afya ni msingi wa maendeleo. Ukiwa na afya njema unaweza kushiriki shughuli za uzalishaji na hata mashindano kama haya ya marathon. Serikali itaendelea kuhakikisha jitihada hizi zinakuwa endelevu," alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema NBC Dodoma Marathon imebeba agenda muhimu ya kitaifa ya kupambana na saratani ya shingo ya kizazi na kuhimiza wananchi kuendelea kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga Taifa lenye afya.

Aidha, ameipongeza Benki ya NBC kwa kutenga shilingi milioni 200 kila mwaka kusaidia utekelezaji wa shughuli za afya kupitia marathon hiyo, pia amezihamasisha taasisi nyingine za sekta binafsi kuiga mfano wa Benki ya NBC kwa kuwekeza katika mipango inayogusa ustawi wa jamii na afya ya wananchi.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mkuu aliwataka waandaaji kuendelea kuikuza NBC Dodoma Marathon ili izidi kuwa tukio kubwa la kimataifa linaloiunganisha Tanzania kupitia michezo, afya na maendeleo ya jamii.

Awali, akitoa taarifa ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi, alisema msimu wa saba wa NBC Dodoma Marathon umeweka historia kwa kuvutia washiriki zaidi ya 15,000, ikilinganishwa na washiriki 1,300 waliojitokeza katika msimu wa kwanza, jambo linalodhihirisha ukuaji mkubwa na kuongezeka kwa imani ya wananchi katika tukio hilo.

Alisema mbio hizo sasa zimetambuliwa rasmi na waandaaji wa mbio maarufu za Comrades Marathon zinazofanyika nchini Afrika Kusini, hatua inayozipa hadhi ya kimataifa na kuifanya Tanzania kuendelea kutambulika katika ramani ya mashindano makubwa ya riadha duniani.

Bw. Sabi alisema NBC Dodoma Marathon inajumuisha mbio za kilomita 42, 21, 10 na 5, na inalenga kuchangisha fedha na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu afya ya mama na mtoto, mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, pamoja na kuboresha huduma maalumu kwa watoto na watu wenye Autism na Down Syndrome.

 Aidha, fedha zinazopatikana zinasaidia mafunzo ya wataalamu wa afya, udhamini wa wakunga na wauguzi wa huduma maalumu ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.

No comments:

Post a Comment