JAMII ZINAZOZUNGUKA MAENEO YA MIGODI ZANUFAIKA NA MIRADI YA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, July 26, 2026

JAMII ZINAZOZUNGUKA MAENEO YA MIGODI ZANUFAIKA NA MIRADI YA MAENDELEO


Na Mwandishi Wetu - Geita


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Nyamwilolelwa na Mtakuja, mradi unaotekelezwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 291,mradi unaotarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wa kike.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Mavunde amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni matokeo ya maboresho ya Sheria ya Madini yaliyoweka wajibu kwa wamiliki wa leseni za madini kurejesha sehemu ya faida kwa jamii zinazowazunguka.

Amesema hatua hiyo imeendelea kuzaa matunda, huku Kampuni ya GGML ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi wa Kata za Nyamwilolelwa, Kijiji cha Nungwe na Mtakuja Mkoani Geita.

Pia, amezindua jengo la kisasa la huduma za mionzi (X-Ray) katika Kijiji cha Kasota, ambalo litasogeza huduma muhimu za uchunguzi wa afya karibu na wananchi wa kijiji hicho pamoja na maeneo jirani. Ujenzi wa jengo hilo umefadhiliwa na Serikali kupitia fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Saragulwa, Waziri Mavunde amesema Serikali imeanza safari ya kutatua changamoto za muda mrefu za wananchi wa eneo hilo kwa kuhakikisha wanapata maeneo ya kutosha kwa shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini kwa utaratibu unaozingatia maslahi ya pande zote.

Aidha, amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Geita kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa fedha nyingi zinazotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeendelea kutumika ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya maji, umeme, barabara na huduma za afya, hali ambayo imehakikisha thamani ya fedha inaonekana kupitia miradi inayowanufaisha wananchi.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Martin Shigela ameishukuru serikali chini ya uongozi wa Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuisimamia kwa ukaribu ili ilete manufaa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment