MHE. KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KITUO CHA AFYA NA DARAJA IGUNGA ASISITIZA AMANI KWA MAENDELEO YA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 8, 2026

MHE. KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KITUO CHA AFYA NA DARAJA IGUNGA ASISITIZA AMANI KWA MAENDELEO YA TAIFA




Na. Veronica Mwafisi-Igunga


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha afya cha Kining’inila na daraja la Nyandekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora huku akisisitiza kuilinda amani ya nchi kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti leo tarehe 08 Julai, 2026 katika maeneo hayo, Mhe. Kikwete amesema maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na ujenzi wa daraja hilo yasingekuwepo kama kungekuwa hakuna amani.

“Tuendelee kufanya kazi kwa bidii, tuitunze amani ya nchi yetu, tumekusanyika hapa kwasababu tuna amani hivyo tusikubali kurubuniwa kuivuruga amani ya nchi yetu.” Amesisitiza.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka kipaumbele katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, miundombinu, maji lengo ni kutaka wananchi wafurahie matunda ya nchi yao.

“Kituo hiki cha afya cha Kiningínila ni mwanzo tu, kwani mpango wa Serikali ni kujenga majengo mengi zaidi ili mpate huduma mbalimbali ikiwemo ya afya ya mama na mtoto, huduma ya meno na nyingine nyingi,” amesisitiza

Aidha, amesema katika Mkoa wa Tabora, Serikali imeajiri watumishi 2200 ikiwemo watumishi wa afya ili wananchi waweze kupata huduma za kitabibu kama ilivyo katika maeneo mengine.

Kuhusu ujenzi wa daraja la Nyandekwa, Mhe. Kikwete amesema daraja hilo litaenda kuondoa adha ya muda mrefu ya kivuko iliyokuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo ya wakazi wa Kijiji cha Manonga na maeneo jirani.

Amesema Mhe. Rais alitoa fedha zaidi ya milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ili kutatua changamoto ya kivuko.

Mhe. Kikwete ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Tabora inayolenga kukagua shughuli za maendeleo katika Mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.










No comments:

Post a Comment