Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema Serikali imejipanga kufanya kazi ili kuhakikisha inatekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara katika Mikoa na Wilaya zote nchini
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Wilayani Butiama mkoani Mara, Dkt.Mwigulu amesema Serikali ilifanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo yenye mahitaji kwa nchi nzima ikiwemo Daraja la Kigongo- Busisi ambapo ilitekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
Dkt.Mwigulu amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuongeza kasi katika utekelezaji wa miundombinu wezeshi ndani ya Mikoa na Wilaya ambapo ameelekeza usanifu wa barabara ya Kitaramanka-Magunga-Busegwe km 37 kuanza haraka na barabara zote za mkoa wa Mara kuwekwa katika utaratibu wa utekelezaji.
“Niwahakikishie Serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kunufaika", amesema Dkt.Mwigulu
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng.Godfrey Kasekenya amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo mkoa wa Mara ambapo ujenzi wa barabara Makutano -Butiama km 50 utekelezaji wake umekamilika.
Amezitaja barabara za Makutano- Butiama -Nyamuswa-fort Ikoma hadi Ngorongoro gate sehemu ya Sanzate-Nata km 40 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 67.
Eng. Kasekenya amesema Serikali imetoa kipaumbele pekee katika utekelezaji wa barabara za Wilaya ya Butiama kutokana na historia ya Baba wa Taifa Mwl.Julias Nyerere Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.






No comments:
Post a Comment