Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema kupitia Kitengo cha Taasisi za Kijinai, imeendelea kubaini mienendo mbalimbali katika jamii inayoweza kusababisha uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Hayo yamebainishwa leo Julai 3, 2026 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Haki Jinai Bw. Constantine Mugusi wakati akizungumza na vyombo vya habari katika banda la THBUB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema baada ya kukusanya taarifa na kufanya tathmini, kitengo hicho hutoa ushauri kuhusu namna ya kuzuia uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
"Baada ya kukusanya taarifa na kufanya tathmini Kitengo hiki kinatoa ushauri wa namna gani tunaweza kuepuka uvunjwaji wa misingi ya utawala bora,"amesema.
Aidha, amesema kitengo hicho kina jukumu la kulinda usiri na usalama wa watoa taarifa, wakiwemo waandishi wa habari, vyanzo vya taarifa, watumishi wanaofanya uchunguzi pamoja na mashahidi.
“Lazima wapewe ulizi ili kulinda usalama wao, kimsingi ni majukumu mapana zaidi lakini yote chimbuko lake ni ushugulikiaji wa malalamiko ya wananchi,"ameongeza.
Bw. Mugusi amesema kuwa kitengo hicho kiliundwa mwaka 2025 kufuatia mapendekezo ya Tume ya Rais iliyolenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi za kijinai nchini.
Kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema masuala ya haki za binadamu ni nguzo muhimu ya maendeleo, hivyo utekelezaji wa dira hiyo unapaswa kuhakikisha hauathiri haki za binadamu wala kukiuka misingi ya utawala bora.
“THBUB inajukumu la kuhakikisha utekelezaji wa Dira 2050 hauathiri haki za binadamu na hauendi kukiuka misingi ya utawala bora katika utekelezaji wake,"amesema. Bw Mugusi.


No comments:
Post a Comment