
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, hatua inayoongeza mvuto kwa wawekezaji wa sekta ya hoteli na kufungua fursa mpya za ukuaji wa utalii na uchumi wa Mkoa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, katika kikao chake na wamiliki wa hoteli kilichofanyika Julai 20, 2026, katika Ukumbi wa Royal Village, jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Senyamule alisema maendeleo makubwa yanayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Dodoma yameufanya kuwa kitovu cha uwekezaji, biashara na huduma mbalimbali, hali inayochochea ongezeko la wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
"Rais ameendelea kuimarisha Mkoa wa Dodoma na kuvutia wawekezaji wengi ambao wameona fursa zilizopo hapa. Wameamua kuwekeza kwa sababu wanaona maendeleo yanayoendelea yanaifanya Dodoma kuwa eneo lenye faida kibiashara na uwezo mkubwa wa kurejesha mitaji yao," alisema.
Alieleza kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, unaotarajiwa kuanza kutoa huduma baadaye mwaka huu, kutaongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi pamoja na mikutano ya kimataifa, jambo litakaloongeza mahitaji ya huduma za malazi na kuchochea uwekezaji katika hoteli za viwango vya juu, ikiwemo zenye hadhi ya nyota tano.
Senyamule pia alisema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuifanya Dodoma kuwa lango la watalii wanaoelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hatua itakayoongeza muda wa wageni kukaa mkoani humo na kuongeza matumizi ya huduma za hoteli, ukarimu na sekta nyingine zinazohusiana na utalii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Hoteli Jijini Dodoma, Gabriel Maunda, alisema wawekezaji wa sekta hiyo wanaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kuboresha huduma na kukuza uwekezaji.
Hata hivyo, alizitaka taasisi hizo kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na kushughulikia changamoto zilizopo ili kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza ushindani na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya hoteli na utalii.





No comments:
Post a Comment